Marekani yadai Urusi na Iran zimejaribu kuingilia kati uchaguzi



Maafisa wa idara ya ujasusi ya Marekani wamesema Urusi na Iran zimetumia taarifa za wapiga kura ili kuwatisha raia wa Kimarekani pamoja na kujaribu kuwafanya wapoteze imani na mfumo wa uchaguzi.


Mkurugenzi wa idara ya ujasusi Marekani John Ratcliffe amesema Jumatano kwamba Urusi na Iran zimejaribu kuingilia kati uchaguzi wa rais unatarajiwa kufanyika rasmi Novemba 3, kwa lengo la kushawishi maoni ya wapiga kura.


Katika mkutano na waandishi habari, uliofanywa ghafla na kwa haraka, Ratcliffe amesema Iran na Urusi zimeweza kupata baadhi ya taarifa za usajili wa wapiga kura, na kuzitumia kusambaza taarifa za uwongo kwa wapiga kura waliojiandikisha ili kuhujumu demokrasia ya nchi hiyo.


Ameongeza kwamba maafisa wa serikali tayari walishagunduwa kwamba Iran imetuma barua pepe zinazolenga kuwatisha wapiga kura, kuchochea machafuko katika jamii na kuchafuwa jina la Rais Donald Trump.


Ratcliffe amevieleza vitendo hivyo kuwa ni vya mahasimu wanaotapatapa. Amesema Marekani itazishughulikia nchi zozote za kigeni zinazoingilia uchaguzi na kwamba maafisa wa ujasusi wameshaanza kujibu tishio hilo. Hata hivyo amewahimiza raia wa Marekani kuchukua tahadhari.


"Ukipokea barua pepe ya kutisha au ya ujanja, usiogope wala usiisambaze," amesisitiza Ratcliffe, na kumtaka kila Mmarekani ajilinde dhidi ya wale aliyowataja kuwa "wanawatakia mabaya."


Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray ambaye alikuwa pamoja na Ratcliffe katika mkutano huo amewaambia wapiga kura wa Marekani waendelee kuwa na imani kwamba kura yako ni muhimu na wala wasiingiwe na wasiwasi kutokana na madai hayo ambayo bado hayajathibitishwa yanayolenga kudhoofisha mfumo wa uchaguzi wa Marekani.


Maafisa hao hawakuweka wazi ni kwa namna gani Urusi na Iran walizipata taarifa hizo. Lakini data za usajili wa wapiga kura ni mali ya umma nchini humo na zinaweza kutikana kiurahishi.


Awali, mashirika ya ujasusi ya Marekani yalionya kuwa Iran inaweza kuingilia kati uchaguzi wa 2020, ili kumuumiza Trump na kwamba Urusi itajaribu kumsaidia Trump katika uchaguzi huo.


Ratcliffe ameitisha mkutano huo wa waandishi habari baada ya wapiga kura wa chama cha Democratic katika majimbo ya Florida na Pennsylvania kuripoti kupokea barua pepe za vitisho zilizoonekana kutumwa na kikundi cha wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia wanaojiita "Proud Boys."

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad