Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC), Dkt. Wilson Mahera, amewaapisha mawakala wa vyama vya siasa 14, ambapo chama cha ACT-Wazalendo pekee ndicho chama ambacho hakina mwakilishi wa uwakala kwa ngazi ya urais.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt.Wilson Mahera amesema kuwa mawakala wa wagombea wa nafasi ya urais ni wawakilishi walioteuliwa na chama baada ya kupata ridhaa ya wagombea wao.
"Wakala wa kujumlisha kura ni mwakilishi aliyeteuliwa na chama baada ya kupata ridhaa ya mgombea, kwa hiyo mliopo humu ndani mmeteuliwa na vyama vyenu baada ya ridhaa ya mgombea, hongereni sana", amesema Dkt. Mahera.
Dkt. Mahera amewaeleza wajibu na majukumu ya mawakala kuwa ni kushuhudia ujumlishaji wa kura za urais, kulinda maslahi ya mgombea na wagombea kwa kuhakikisha sheria, taratibu na kanuni zinafuatwa wakati wa kujumlisha matokeo ya uchaguzi na wanao wajibu wa kusaini fomu ya matokeo ya uchaguzi.
"Si kuhesabu kura tu bali kufuata sheria na kanuni zote za wakala na ukienda ndivyo sivyo utawajibika kama sheria inavyosema” amesema Dkt. Mahera.