Aisha Jumwa alivamia nyumba ya mpinzani wa kisiasa kukabiliana na wafuasi wanaompinga wakati tukio hilo lilipotokea.Image caption: Aisha Jumwa alivamia nyumba ya mpinzani wa kisiasa kukabiliana na wafuasi wanaompinga wakati tukio hilo lilipotokea.
Mbunge mmoja nchini Kenya amekuwa kizuizini kwa siku tatu akisubiri matokeo ya vipimo vya uchunguzi wa akili kabla ya kusikilizwa kwa mashtaka ya mauaji dhidi yake.
Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa alifikishwa mahakamani huko Mombasa. Mwendesha mashtaka alisema ana ushahidi wa kutosha wa kumshtaki mbunge huyo dhidi ya mauaji ya Ngumbao Jola yaliyotokea mwaka 2019.
Bwana Jola alipigwa risasi wakati wa ghasia zilizotokea kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa kata eneo bunge la Malindi linalowakilishwa na Aisha Jumwa.
Imeripotiwa kwamba Bi. Jumwa alikuwa amevamia nyumba ya mpinzani wake wa kisiasa kukabiliana na wafuasi wanaompinga wakati tukio hilo linatokea.
Matokeo yakionesha yuko sawa kushtakiwa, atafikishwa mahakamani siku ya Alhamisi.
Kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, wakosoaji wameshtumu serikali kwa kumshurutisha Bi. Jumwa kwa sababu ya msimamo wake wa kisiasa.
Mbunge huyo ametangaza kumuunga mkono makamu rais Wiliam Ruto.
Jumwa pia anakabiliwa na madai mengine ya ubadhirifu wa fedha za maendeleo ya eneo karibu dola 20,000.
Wabunge kadhaa wanachunguzwa kwa madai ya ufisadi na uhalifu mwingine. Juni mwaka huu, mbunge John Waluke alihukumiwa kifungo cha miaka 67 jela kwa makosa ya ufisadi, au alipe faini ya dola milioni 7.
Baada ya kuwa gerezani kwa karibu miezi minne, alipewa dhamana alikisubiri kusikilizwa kwa rufaa aliyowasilisha.