Mchumba wa mwandishi wa Saudia Jamal Khashoggi aliyeuawa nchini Uturuki amewasilisha kesi mahakamani dhidi ya mwanamfalme wa Saudia, akimtuhumu kwa kuagiza mauaji hayo.
Hatice Cengiz na makundi ya wanaharakati ya haki za kibinadamu yalioanzishwa na Khashoggi kabla ya kifo chake yanamshtaki mwanamfalme Mohammed bin Salman na zaidi ya watu wengine 20 kwa kiwango cha uharibifu kisichojulikana.
Khashoggi aliuawa na kundi la mawakala wa Saudia wakati wa ziara yake katika ubalozi wa Saudia mjini Instabul, Uturuki 2018.
Mwanamfalme huyo amekana kutekeleza mauaji hayo.
Khashoggi alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudia na alikuwa akiishi mafichoni nchini Marekani, mara kwa mara akiliandikia gazeti la The Washington Post.
Katika kesi hiyo iliowasilishwa mjini Washington siku ya Jumanne, raia wa Uturuki bi Cengiz anadai kuathiriwa binafsi na kifedha kufuatia kifo cha Khashoggi.
Kundi la kupigania haki za kibinadamu la, Democracy for the Arab World Now (Dawn), linasema kwamba operesheni zake ziliathirika.
Mashtaka hayo yanadai kwamba Khashoggi aliuawa ''kufuatia maagizo kutoka kwa mshukiwa Mohammed bin Salman".
"Lengo jingine la mauaji hayo lilikuwa wazi - Kumzuia bwana Khashoggi kupigania mabadiliko ya kidemokrasia katika ulimwengu wa Waarabu akiwa nchini Marekani'', ilisema kesi hiyo.
Katika mkutano uliofanyika kupitia video siku ya Jumanne, mawakili wa bi Cengiz na Dawn walisema kwamba lengo la kesi hiyo ni kuilazimu mahakama ya Marekani kumwajibisha mwanamfalme huyo kwa mauaji hayo na kupata stakhabadhi zinazoonesha ukweli, kulingana na gazeti la The Washington Post.
''Jamal aliamnini kwamba kila kitu kinawezekana Marekani na sasa naweka imani yangu chini ya mfumo wa mahakama ili kupata haki na uwajibikaji'', bi Cengizi alisema katika taarifa yake.