WIKIENDI iliyopita, ulipigwa mchezo wa kimataifa wa kirafi ki kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo ilikuwa mwenyeji wa Timu ya Taifa ya Burundi. Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar, Taifa Stars ilikubali kipigo cha bao 1-0.
Ukiangalia taswira nzima ya mchezo ule, Taifa Stars walikuwa vizuri kwa takribani dakika 80 wakifanikiwa kuutawala mchezo, lakini umakini mdogo wa safu ya kiungo na ulinzi ukaigharimu timu kwa kufanya kosa lililozaa bao la ushindi kwa Burundi. Kabla ya hapo, safu ya ushambuliaji ilikosa mabao kadhaa.
Novemba 13, mwaka huu, Taifa Stars itakuwa mgeni wa Tunisia kwenye mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzAa kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2022) mchezo utakaopigwa kule jijini Tunis nchini Tunisia.
Ukiwaangalia Tunisia ni moja ya timu bora na tishio Afrika, hivyo tahadhari kubwa kuelekea mchezo huo inatakiwa kuchukuliwa
Benchi la ufundi la Taifa Stars chini ya Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije na wasaidizi wake, Juma Mgunda na Seleman Matola wanapaswa kuyafanyia kazi makosa ya kiufundi yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita ili kuepusha athari zaidi kwenye mchezo ujao ambao ni muhimu kwa taifa kwani ni ndoto yetu kushiriki tena michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo.
Kikosi cha stars kimesheheni nyota wenye vipaji vya hali ya juu ambao wana uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu, hivyo ni wajibu wao kujua thamani ya jezi ya timu ya taifa, mnapaswa kupambana kwa nguvu zenu zote kuhakikisha ndoto ya Watanzani inatimia kwa mara nyingine.
Ni jambo jema kuona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeunda kamati ya hamasa na ushindi ambayo itasaidia kuongeza morali kwa wachezaji kujituma na kupambana uwanjani, kamati pia ihakikishe inafanya kazi yake kwa ufanisi wa hali ya juu kwani jukumu walilopewa ni kuhakikisha timu ya taifa inashinda kila mchezo.
Wachezaji mnaporudi kwenye klabu zenu hakikisheni mnafanya mazoezi na kujituma kwa hali ya juu ili mnapokuja kwenye timu ya taifa muendeleze kile mnachokifanya kwenye timu zenu.
Watanzania kila mmoja anatakiwa kujitoa kwa ajili ya timu ya taifa na tuungane kukemea viashiria vyovyote ambavyo vinaweza kutugawa kama taifa, utofauti ubaki kwenye klabu mnazozisapoti, lakini linapokuja suala la timu ya taifa tuhimize umoja wetu.
Mamlaka husika zinapaswa kuwaandalia mazingira bora wachezaji kuelekea mchezo dhidi ya Tunisia ili kuwaongezea morali ya kupambana kwenye mchezo huo mgumu kutokana na aina ya timu nambayo tunakutana nayo.
Linapokuja suala la wachezaji kuingia kambini pia wanapaswa kuwahi ili kutochelewesha program za mwalimu.Kwa upande wa kocha mkuu aendelee kufuatilia mechi mbalimbali za ligi tofauti ili kupata wachezaji wenye ubora ambao watapambana kwa ajili ya taifa hapo Novemba 13 kule Tunisia.
Tukumbuke kuwa, Taifa Stars ipo Kundi J, baada ya kucheza mechi Novemba 13 dhidi ya Tunisia, timu hizo zitarudiana Novemba 17, mwaka huu jijini Dar. Tunahitaji kufanya vizuri, hivyo tushirikiane.