DAR: Wakati zikiwa zimesalia siku moja kabla ya Watanzania kufikia kilele cha Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu, Mgombea Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe ametakiwa kurejea CCM baada ya kushindwa kuhimili mikiki ya upinzani.
Hatua hiyo imekuja baada ya mgombea huyo kufanya kampeni kwa kusuasua kwa muda wa wiki mbili pekee na baadaye kushindwa kabisa kuendelea na kampeni hizo hadi sasa huku viongozi wakuu wa chama hicho wakitangaza kumuunga mkono Mgombea Urais wa Chadema, Tundu Lissu.
Mapema wiki iliyopita mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad aliweka wazi kuwa, nia ya Membe ni kutaka kuwachanganya Watanzania, lakini msimamo wa ACT-Wazalendo ni kumuunga mkono Lissu.
Maalim Seif alitoa msimamo huo baada ya Membe kuapa kuendelea na kampeni zake za urais kupitia ACT Wazalendo.
“Nataka kufunga bao dakika ya 89 kutokea benchi. Watanzania mkae macho na mkae chonjo. Tumefanya kazi huku chini, sasa tunakuja juu kupata bao la ushindi dakika ya 89 na dakika za nyongeza,” ni kauli ya Membe alipozungumza na waandishi wa habari mapema wiki hii.
Hata hivyo, Maalim Seif alieleza kusitikishwa na kauli hiyo ya Membe kwa kuwa vikao vilivyopitisha azimio la kumuunga mkono Lissu, Membe alishiriki.
“Naye (Membe) akatuhakikishia kwamba anakubali tumuunge mkono Lissu. Hivyo, kamati ya uongozi kwa kauli mmoja akiwemo Membe tukakubaliana, tumuunge mkono Lissu.
“Niseme nasikitika sana kwa aliyozungumza ndugu yangu Membe jana. Chama chetu cha ACT-Wazalendo, kupitia mkutano mkuu wa Taifa, uliamua kwamba tunataka mabadiliko katika nchi yetu, na kama vyama makini havutashirikiana, itakuwa ni vigumu kuoindoa CCM madarakani.
“Kwa hivyo, Mkutano Mkuu wa Taifa ukatoa madaraka kwa Halmashauri Kuu, Kamati Kuu na Kamati ya Uongozi na kuhakikisha ACT-Wazalendo inafanya kila juhudi ili kuhakikisha tunashirikiana na wenzetu katika vyama ambavyo ni makini,” alisema Maalim Seif.
“Ndugu Membe alipokuja kwenye chama chetu, tulimwambia mapema kabisa, maamuzi ya Mkutano Mkuu, tutashirikiana na vyama vingine. Je mwenzetu, unachukua nafasi hii tukiamua kushirikiana na vyama vingine, utakubali? akasema naam nitakubali,” alisema.
Maalim Seif alisema mgombea wao, (Membe) haonekani… ni afadhali mzee wa ubwabwa (Hashim Rungwe- Chauma) anaonekana.
AREJEE CCM
Kutokana na hali hiyo baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa wamesema umefika wakati sasa wa Membe kuomba kurejea CCM.
Wachambuzi hao walisema Membe hana pa kushika kwa sasa hasa ikizingatiwa viongozi wakuu wa chama chake, (Maali Seif, Zitto Kabwe) wameona hana nguvu kisiasa kama aliyonayo Lissu.
Mmoja wa wachambuzi hao, Mpoki Buyah alisema hatua Membe kusuasua katika kampeni hizo, imedhihirisha wazi kuwa mgombea huyo hana mvuto wa kisiasa katika upande wa upinzani.
“Kwa kuwa ameshapima kina cha maji na kuona hawezi kuvuka, arudi alikotoka ili asije kuzama kabisa, tunaona huku upinzani hana tena pa kushika, chama chake kinamuona hafai, Chadema ndio hivyo tena hawana muda naye, sehemu pekee salama kwake ni CCM,” alisema.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Godfrey Matemba mchambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa, ambaye pamoja na mambo mengine, alisema ili Membe astaafu kwa heshima inabidi arejee CCM.
CCM: TUNAMKARIBISHA
Aidha, akizungumzia misukosuko hiyo ya Membe, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga aliliambia IJUMAA kuwa ni dhahiri Membe amedhalilika.
Alisema kwa kuwa Membe alikuwa kada mkongwe wa chama hicho, anafahamu taratibu zote za kufuata ili arejee CCM.
“Kweli heshima yake imeshuka kama anafananishwa na Mzee wa Ubwabwa! Sisi tunamkaribisha lakini afuate taratibu za chama kwa sababu anafahamu taratibu zote.
“Baada ya hapo CCM itakaa na kufuata taratibu zote kumrejesha kwa mujibu wa taratibu na katiba ya chama,” alisema.
Kauli hiyo ya Kanali Lubinga inashabihiana na kauli aliyowahi kutoa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally siku chache baada ya Membe kutimuliwa CCM.
Bashiru alieleza kuwa milango ya CCM kupokea wanachama wanaokiri makosa yao na kuomba msamaha iko wazi, hivyo Membe anaweza kukata rufaa juu ya kufukuzwa kwake.
“Mchakato huu ni kama wa kimahakama kuna rufaa, nikianza mimi kusema wakati mimi ndio nitapokea rufaa kama nipo ni kama naingilia mchakato wa haki. Na matarajio yangu ni kwamba atarudi CCM, nikiwa hai au nimekufa.
“Sababu milango ya kuwapokea wanachama iko wazi na kuondoka iko wazi, mimi nimesaini barua za misamaha 14 na niko tayari kusaini ya Membe kurudi kama akitaka,” alisema Dk. Bashiru.
Stori: Gabriel Mushi, Ijumaa