Mimba ya Aunt Hatarini!



KITENDO cha staa wa filamu za Kibongo, Aunt Ezekiel kunaswa ‘club’ ya starehe ya usiku akigida pombe za hatari ilihali ni mjamzito wa kujifungua muda wowote, kimeibua gumzo kubwa juu ya hatari ya kuchoropoka kwa mimba hiyo.

Wikiendi iliyopita, Aunt alinaswa akitandika bia kama zote kwenye Club ya The Base iliyopo Makumbusho jijini Dar, usiku wa manane ambapo kulikuwa na shoo ya msanii wa Bongo Fleva anayedaiwa ndiye mwenye ujauzito huo aitwaye Salmin Said ‘Kusah’.

Bila kujali ukubwa wa kitumbo chake, pia Aunt ndiye alikuwa MC wa shoo hiyo kabla ya kuweka kambi kwenye moja ya kona na kuanza kutandika ulabu aina ya bia ambazo zina sifa ya kuwa na kilevi kikubwa.

Hata hivyo, baada ya ishu hiyo kuibua mjadala mkali, gazeti hili liliibeba hadi kwa daktari ambaye amefunguka kinagaubaga juu ya madhara ya unywaji wa pombe kwa mwanamke mjamzito kama Aunt. Dk Geofrey Charles ‘Dk Chale’ ni daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na watoto ambaye anasema kuwa, mama kutumia kilevi wakati wa ujauzito, kunaweza kusababisha mimba kutoka au kuzaa mtoto ambaye ana matatizo hivyo kwa staa huyo kunywa pombe hadharani na hata mafichoni siyo sahihi.

“Hakuna sehemu yoyote inayoruhusu mjamzito kunywa pombe hata kidogo. Ni hatari kwa afya ya mtoto aliyepo tumboni, lakini pia kuna uwezekano mkubwa wa mimba kutoka,” anasema Dkt. Chale akimtahadharisha Aunt kuachana na pombe kwenye kipindi hiki cha ujauzito na kuongeza;

“Anatakiwa aelewe kwamba pombe ni sumu kwa mtoto. Mjamzito anapokunywa pombe inaingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa damu wa mama kisha hufika kwa mtoto kupitia kondo la nyuma (placenta).


“Pombe inapoingia kwenye mzunguko wa damu wa mtoto, huathiri uwezo wa mtoto kupata chakula, virutubisho na oksijeni ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya kawaida katika ubongo na viungo vingine. Hii inaweza kuathiri ubongo wa mtoto na ukuaji wa viungo vya mwili kwa jumla.

“Uharibifu huu unaweza kuathiri uwezo wa mtoto kujifunza na kufikiri pale anapozaliwa, hali ambayo itajionesha kwa matendo yake kama mtoto na kama mtu mzima.


“Utafiti unaonesha kwamba, uwezo wa mimba kustahimili kiwango cha pombe ni mdogo mno hali ambayo huathiri ufanyikaji wa viungo na ukuaji wake kwa kiasi kikubwa, hivyo kunakuwa na hatari ya mimba kutoka.

“Kama mtoto akizaliwa, madhara haya yanaweza kusababisha kifo kwa mtoto, malezi na makuzi ya taabu na hata hisia mbalimbali katika maisha.

“Kwa mjamzito yeyote, ni vizuri kuacha kunywa pombe.”

Kwa upande wake, Aunt, katika mazungumzo na gazeti hili juu ya ishu hiyo, alisema kuwa anachojua pombe inaongeza damu.


“Mimi ninachojua pombe inaongeza damu siku zote, kwa hiyo ninakunywa kwa afya na siyo kupitiliza kama watu wanavyofikiria,” anasema Aunt ambaye anatarajia kupata mtoto wa pili baada ya yule wa kwanza, Cookies aliyezaa na Moze Iyobo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad