Wagombea wawili wa Ubunge wa majimbo ya Ndanda na Tandahimba, waliokuwa vyama vya upinzani na kuhamia Chama cha Mapinduzi, (CCM), Cecil Mwambe na Katan Ahmed Katan, wameeleza machungu waliyokuwa wakikumbana nayo wakati wakitaka kuwatumikia wananchi wao.
Wabunge hao wametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa kuwanadi wagombea ubunge na udiwani wa CCM, uliofanyika wilayani Masasi na kuwaonya wakazi hao wasifanye makosa ya kuchagua wapinzani kwani wataendelea kukosa maendeleo.
"Mambo yaliyokuwa yanafanyika huku Masasi hata sisi kule Ndanda tulikuwa tunayatamani, hii ni kwa sababu hakuna cha maana kule kilichoandikwa kwa ajili yenu na mimi ni shahidi, katika miaka mitano ya ubunge wangu, sijawahi kuitikia ndiyo na madhara yake nimeyaona, ninawaomba sana, msifanye makosa hayo", amesema Mwambe.
"Ukienda Bungeni kutaka kusema Masasi tuna shida ya umeme, wakubwa wanasema kapinge bajeti, tutaupataje umeme? tumekwenda Bungeni tumepiga plasta, sasa ukitaka kuomba umeme, utaongea vipi na wewe midomo umeifunga plasta?", amesema Katani.