JESHI la Polisi Mkoa wa Manyara linawashikilia watu saba kwa ajili ya uchunguzi zaidi kutokana na tukio la mauaji ya Manace William Lemoringeti, ambaye alikuwa mlinzi wa mgodi wa bilionea Saniniu Laizer mkoani Manyara.
Akizungumzia tukio hilo, mdogo wa marehemu, Loshii William Lemoringeti, ameiomba serikali kuingilia kati suala hilo hasa jeshi la polisi ili kupata ukweli wa chanzo halisi cha kifo cha ndugu yao kabla ya maziko.
“Mpaka sasa hatujapanga maziko kwa sababu polisi hawajaturidhisha na maelezo yao, tunaendelea kusikiliza polisi na Serikali wanatueleza nini. Kwa maelezo yao wanasema amekufa akiwa camp mgodini, wanasema alikuwa mlinzi wa mgodi wa bilionea Laizer na hakuwa peke yake, alikuwa na wenzake, fensi wala geti havijavunjwa.
“Amekutwa amekatwa kwa shoka wala hajajifurukuta, hata mbuzi au kuku ukimchinja lazima atajifurukuta, inaonekana aliondolewa eneo la tukio kwa hiyo huenda walimuua wakamhamisha, walitumia vigezo vipi kumhamisha usiku kumpeleka hospitali, polisi na jeshi wapo, inaonekana kuna kitu alifanyiwa wakamuondoa kupoteza ushahidi,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Paul Kasabago amesema:
“Tukio hilo nalifahamu, mtu huyo aliuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana, wakatoweka. Watu saba wamekamatwa kwa ajili ya uchunguzi, mwili umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi,” amesema SACP Kasabago.