Mondi Mfalme wa Kukopi na Kupesti?

 


MUZIKI mzuri hutengenezwa na ubunifu, ambao utaifanya kazi ya msanii kuishi miaka mingi na kusikilizwa au kutazamwa na vizazi vyote ambavyo, vinafuatilia na kupenda burudani.

 

Lakini tasnia ya muziki hapa nchini, imekuwa ikikumbwa na kasumba moja ya baadhi ya wasanii kukopi na kupesti kazi za wasanii wa nje.


Hii inaweza ikawa ni kwenye mdundo, mavazi, mashairi na hata ubunifu wa kazi hizo. Jambo hili limekuwa likionekana siku hadi siku kwa baadhi ya wasanii Bongo.


Katika kukopi huko, kumekuwa na faida na hasara, ambazo zinatokea baada ya msanii kukopi kazi ya msanii wa nje.

 

Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’, ni staa mkubwa wa muziki barani Afrika. Ni bosi wa lebo ya muziki ya Wasafi Classic Baby (WCB) ambayo imetoa wasanii wakubwa kama Rajab Abdul ‘Harmonize’, Richard Martin ‘Rich Mavoko’, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, Mbwana Yusuf ‘Mbosso Khan’, Abdul Idd ‘Lava Lava’, Zuhura Othman ‘Zuchu’ na Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’.

 

Mondi anasifika kwa kuachia kazi kali, ambazo zinakimbiza kwenye mitandao ya kuuza na kusikiliza muziki (platforms) na kushika nafasi za juu (trending).


Lakini katika nyimbo hizo, Mondi amekuwa akituhumiwa kukopi na kupesti baadhi ya ngoma za wasanii wengine. Inaweza ikawa ni kwenye mdundo, video, mashairi na hata mavazi.


Inaweza ikawa na faida kwake kwa kuwa kazi zake zinazidi kutikisa na kufuatiliwa zaidi sehemu mbalimbali duniani.

 

Lakini mbali na faida za kukopi na kupesti, pia kunaweza kukawa na hasara zake, ambazo ni kazi hizo kushuka hadhi kwa nchi za nje, kwani Bongo Fleva inapaswa kufuatiliwa kutokana na ubunifu wa Kibongo, lakini kama ni kukopi nchi za nje, na wao ni sehemu ya wafuatiliaji wa muziki huo, inakuwa ni kazi bure au itakuwa ngumu kutoboa na kuvuka mipaka ya Bongo.

 

OVER ZE WEEKEND inakudadavulia baadhi ya ngoma na video, ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwamba, Mondi amekopi na kupesti kutoka kwa wasanii wengine, hivyo kukosolewa mara kwa mara na kuambiwa ameishiwa ubunifu;

 


CHECHE NA NAUGHTY GIRL YA BEYONCE

Cheche ni ngoma ya memba mpya wa Wasafi, Zuchu akiwa na bosi wake, Mondi ambayo ilikimbiza na bado inakimbiza kwa kushika nafasi ya juu kwa muda mrefu mitandaoni, ikiwemo YouTube.


Kwenye Cheche, Zuchu na Mondi wamekopi baadhi ya vitu kutoka kwenye Ngoma ya Naughty Girl ya mwaka 2003 ya mwimbaji wa RnB wa Marekani, Beyonce Knowles akiwa amemshirikisha Usher Raymond.




MAVAZI; Ni kipengele ambacho kimeonekana kukopiwa na kufanana na ngoma hiyo, kwani jinsi alivyovaa Usher, ndivyo alivyovaa Mondi na hata upande wa Zuchu, amekopi na kufanana kimavazi na Beyonce.


LOCATION; Hiki ni kipengele kingine ambacho Mondi na Zuchu wamekopi kutoka kwa Beyonce, kwani location ya club iliyotumika kwenye Naughty Girl, ndiyo imeonekana kutumika kwenye Ngoma ya Cheche.


UBUNIFU; Ubunifu wa kucheza kwenye Ngoma ya Naughty Girl, ndiyo uliyotumika kwenye Ngoma ya Cheche. Usher anaonekana akivuta sigara kwenye ngoma hiyo, na ndivyo alivyofanya Mondi kwenye Cheche.


 


BABA LAO NA SOAPY YA NAIRA MARLEY


Baba Lao ni miongoni mwa ngoma kubwa za Mondi, ambayo aliiachia miezi kumi na moja iliyopita na kufanya poa mitandaoni. Lakini skendo kubwa juu ya ngoma hiyo, ni kwamba alikopi mdundo (beat) kutoka kwa msanii wa nchini Nigeria, Naira Marley.


 


Mdundo uliotumika kwenye Ngoma ya Baba Lao, ndiyo mdundo halisi wa Ngoma ya Soapy ya Naira.


Katika mazungumzo ya prodyuza wa ngoma hiyo, S2kizzy ambaye amekuwa akitengeneza ngoma za Mondi, alisikika akisema kuwa, hawakuiba mdundo huo, bali yalikuwa ni makubaliano baina ya Mondi na Naira, hivyo mashabiki wasishangae kuona wawili hao, wakitoa remix au ngoma ya pamoja.



GERE NA BRISA YA IZA


Gere ni ngoma ya mwanamama na staa mkubwa wa muziki kutoka nchini Kenya, Tanasha Donna akiwa ameshirikiana na baba mtoto wake ambaye ni Mondi.


 


Katika ngoma hiyo, wawili hao wanatuhumiwa na msanii kutoka nchini Brazil, Iza kuwa wamekopi video ya ngoma yake ya Brisa.


Katika video ya Gere ambayo imetoka miezi saba iliyopita, imeonekana kukopi na kufanana baadhi ya vitu na Ngoma ya Brisa kuanzia mavazi na hata location kwa asilimia kubwa.


 


TETEMA NA SEE YOU AGAIN YA TYLER CREATOR


Tetema ni ngoma ya memba wa Wasafi, Rayvanny akiwa amemshirikisha bosi wake, ambaye ni Mondi.


Ngoma hiyo ambayo ina mwaka mmoja tangu ilipotoka, ilikutana na tuhuma za kukopi na kufanana baadhi ya vipande (scene) na video ya See You Again ya rapa mkali wa nchini Marekani, Tyler Creator.





FIRE NA SWALLA YA JASON DERULO


Fire ni ngoma ya Mondi akiwa amemshirikisha Tiwa Savage wa Nigeria.


Katika Ngoma ya Fire yenye miaka mitatu sasa, Mondi alikopi video ya Ngoma Swalla ya Jason Derulo, akiwa na Nick Minaj.


Baadhi ya vipande vya video ya Ngoma ya Fire, vimekopiwa au vinafanana na vile vya kwenye video ya Swalla.


BAILA NA SAANS YA SHARUK KHAN


Baila ni ngoma ya Mondi aliyomshirikisha mshindi wa tuzo kubwa ya Grammy kutoka nchini Marekani, Miri Ben -Ari.


 


Baila ambayo ina miaka miwili sasa tangu ilipotoka, Mondi alikopi baadhi ya vipande (scene) kwenye video ya mwigizaji mkali wa Bollywood nchini India, Sharuk Khan.


Saans ambayo ilikuwa ni sound track ya filamu ya Sharuk Khan, imeonesha kukopiwa takriban vitu vyote, ikiwemo scene za video hiyo.





LITAWACHOMA NA EAT YA TOBE NWIGWE


Litawachoma ni ngoma mpya ya Zuchu akiwa na Mondi na inakimbiza kwa sasa mitandaoni, kiasi cha kushika namba 83 kwenye orodha ya video kali duniani kote.


Litawachoma imekopi na kufanana baadhi ya vipande vya video kutoka kwenye Ngoma ya Eat ya rapa mwingine wa Marekani, Tobe Nwigwe.





JEJE NA JORO YA WIZKID


Jeje ni ngoma ya Mondi ambayo ilitoka miezi kadhaa iliyopita na bado inaendelea kufanya poa kwenye mitandao yote ya kuuza na kupakua muziki.


 


Jeje imekopi na kufanana baadhi ya vitu kutoka kwenye Ngoma ya Joro ya Wizkid wa Nigeria, ambayo ilitoka mwaka 2019. Ukisikiliza vizuri ngoma hizo kwa upande wa saundi, zinafanana.


 


Mambo haya ya kukopi na kupesti, yameendelea kufukuta kila kukicha, hasa Mondi anapoachia ngoma mpya, huku akipewa majina mbalimbali likiwemo la Mfalme wa Kukopi na Kupesti!


Makala: HAPPYNESS MASUNGA

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad