MSAFARA wa mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu umepigwa mawe na watu wasiojulikana Chato mkoani wa Geita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).
Kadhia hiyo imetokea jana jioni Jumanne tarehe 13 Oktoba 2020 mara baada ya Lissu kumaliza kuhutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Chato Mjini.
Moja ya gari limeharibiwa kioo kwa jiwe lililorushwa na watu wasiojulikana wakati msafara huo wa Lissu ukiondoka wilayani humo.
Lissu alisema kuna baadhi ya watu walimrushia mawe yeye na wafuasi wake, wakati wanaondoka baada ya kumaliza mkutano huo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020.
“Tumekuja kufanya mkutano kwa mujibu wa ratiba yetu ya tume, kuna wahuni wamekodiwa kutufanyia fujo, jeshi halijafanya chochote kuwadhibiti, tumemaliza mkutano tunaondoka tumerushiwa mawe sana,” alisema Lissu.
Kutokana na hatua hiyo, Lissu alitaka magari yaliyokwa kwenye msafara wake, yafunge barabara hadi pale gari la matangazo litakapofika eneo walilokwa wakihofia kuharibiwa hali iliyosababisha mvutano na polisi.
“Na tunahofia watachoma moto gari ya matangazo, tunabaki hapo tunasubiri polisi watulinde, mawe yanaendelea kurushwa hatutaondoka hapa.”
“Kama ni kudhibiti nguvu ya umma kumuondoa madarakani tutabaki hapahapa nyumbani kwake tupigwe mawe. Hapo tumekuja nyumbani kwa Rais, Watanzania wafahamu, dunia ifahamu,” alisema Lissu.
Baada ya kusubiri kwa muda, gari hilo lilifika eneo hilo na msafara ukaendelea licha kwamba ulipokuwa umefunga barabara kulisababisha adha kwa watumiaji wengeni.