Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikizidi kushika kasi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Mstaafu Francis Mutungi amewataka wadau wote wa uchaguzi wakiwemo wanasiasa kuepuka misuguano na Serikali.
Jaji Mutungi ametoa rai hiyo leo katika kikaao cha pamoja na wadau wote wa siasa kilichofanyika Jijini Dar es Salaam akieleza kuwa yeye kama mlezi wa vyama hafurahishwi na baadhi ya kauli za vyama vya siasa kupitia wagombea wao ambazo ni dhahiri zinaenda kinyume na kanuni za maadili ya uchaguzi walizosainishwa na tume ya uchaguzi.
Amesema katika siku hizi chache za kampeni zilizosalia ni muhimu mno kuepuka migongano akishauri wadau kuwa kwa mwenye malalamiko yeyote kuhusu uchaguzi ni vyema akafika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo ndiyo inaratibu masuala yote ya uchaguzi.
"Sisi hapa tukianzisha vurugu tunauwezo wa kupanda ndege habari gani kuhusu wengine ambao hawana hili wala lile Vipi kuhusu watoto na makundi mengine", amesema Jaji Mutungi.
Aidha, amesema ofisi ya msajili imekuwa ikitoa maonyo kwa baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa vikikiuka taratibu za usajili, huku akitoa wito kwa wafuasi wa vyama kulinda amani kwa kuwa yapo maisha baada ya uchaguzi.