Polisi mmoja wa zamani katika mji wa Minnesota, aliyefunguliwa mashitaka ya mauaji ya mwanaume mweusi akiwa chini ya ulinzi wa polisi amepewa dhamana. Derek Chauvin, mwenye umri wa miaka 44, ambaye anakabiliwa na mshitaka ya kuua bila kukusudia katika tukio la Mei 25, la kifo cha George Floyd, mwenye umri wa miaka 46, aliachiwa kwa dhamana ya dola milioni moja, Jumatano. Chauvin pia anakabiliwa na mashitaka ya kiwango cha tatu cha mauaji, na mauaji ya kutokusudia. Katika video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, Chauvin, alirekodiwa akiwa amemuwekea goti George Floyd, kwa takriban dakika tisa, huku Floyd ambaye alikuwa amefungwa pingu akisema mara kwa mara “siwezi kupumua.” Tukio hilo lilichochea maandamano makubwa, na ghasia mjini Minneapolis, kote Marekani, na duniani.