IMEWASHTUA watu, duka la nguo za watoto la Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, kufungwa.Duka hilo linaloitwa Little Sweethearts, ambalo lipo Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar es Salaam, siku za hivi karibuni, limekuwa halifunguliwi huku sababu lukuki zikitajwa.
“Niko bize nashuti,” Wema alipokea simu ya waandishi wetu kwa maneno hayo, kabla hajasikiliza sababu za kupigiwa simu.
Awali chanzo chetu kilichokaribu na miss huyo, ambaye pia ni msanii, kilidai kuwa duka limefungwa, kutokana na Wema kushindwa kulipa kodi ya pango.
Kiguu na njia cha waandishi wetu, kiliwafikisha hadi kwenye duka hilo na kushuhudia likiwa limefungwa, lakini ukweli wa mrembo huyo kukwama kulipa kodi, ukabaki kuwa mtihani.Wafanyabiashara wengine waliokaribu na duka hilo, walipoulizwa na waandishi wetu, walisema: “Hata sisi tumeona hafungui, sasa kama ni kodi au sababu nyingine, hatujui.”
Majibu hayo yaliwapeleka waandishi wetu, katika kumtafuta mmiliki wa ‘fremu’ hiyo ili kumuuliza kama anamdai Wema kodi ya pango, lakini jitihada ziligonga mwamba.
Rafiki wa Wema ambaye amekuwa akishirikiana naye kibiashara, amesema alipoulizwa na waandishi wetu:“Kuna changamoto za kibiashara zinazomkabili Wema, zikiisha atafungua.”
Hata hivyo, rafiki huyo ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini, hakuzitaja changamoto hizo ni zipi na lini zitatatuliwa ili wanaoshtuka na kufungwa kwa duka hilo, watulize mioyo yao.
Mmoja kati ya wafanyabiashara wa nguo waliopo karibu na duka hilo, aliliambia Risasi Jumamosi kuwa, wateja bado wanaendelea kufika dukani hapo, lakini hawapati huduma.
“Ukifunga duka kwa muda, unapoteza wateja. Kama Wema bado ana mpango wa kuendelea na biashara hii, ni vyema akamaliza mambo yake mapema,” alisema mfanyabiashara huyo ambaye takwa la jina lake kuhifadhiwa, limezingatiwa.
Aidha, kusanya taarifa ya waandishi wetu, ilijaa madai mengi yanayochangia mrembo huyo kushindwa kufungua duka lake, yakiwemo ya mtaji kukata, kuandamwa na madeni na kutoswa na aliyekuwa akimsapoti, huku suala la kukosa muda, nalo likitajwa.
Siku za hivi karibuni, Wema aliachana na maisha ya ‘janjajanja za mjini’ na kujikita katika biashara, ambapo kwa sasa pia amejikita kwenye suala la uigizaji, ambalo huwenda nalo linamchukulia muda mwingi wa kushindwa kushika mawili kwa mpigo.