Dar es Salaam. Bondia bingwa wa mabara wa uzito wa superwelter Hassan Mwakinyo atautetea mkanda wake wa Chama cha WBF Novemba 13 dhidi ya bondia wa Argentina Jose Carlos Paz.
Pambano hayo yamepewa jina la Dar Fight Night yameandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports.
Mbali ya kutetea mkanda huo, Mwakinyo pia atawania ubingwa wa mabara wa uzito huo huo wa Chama cha IBA. Pambano hilo limepangwa kufanyika kwenye ukumbj wa Next Door Arena.
Mkurugenzi wa The Jackson Group Sports Kelvin Twissa amesema siku hiyo mabondia kutoka nchi tano watazichapa kumsindikiza Mwakinyo na Paz, akiwamo aliyekuwa bingwa wa dunia wa WBC, Fatuma Zarika kutoka Kenya.
Twisa alisema kuwa Zarika atazichapa na Patience Mastara wa Zimbabwe, na Zulfa Yusuph Macho atacheza na Alice Mbewe wa Zimbabwe.
Pia siku hiyo, bondia Abdallah Pazi maarufu kwa jina la Dullah Mbabe atacheza na Alex Kabangu wa DR Congo.
Alisema kuwa wameamua kuingia kwenye mchezo wa ngumi kutokana na kutambua vipaji vya mabondia mbalimbali hasa Mwakinyo ambaye anafanya vizuri katika mapambano yake.
"Siku hiyo kutakuwa na pambano makubwa ambapo mabondia kutoka nchi sita, Argentina, DR Congo, Kenya, Uganda, Zimbabwe na wenyeji Tanzania watapigana, ni siku ambayo mashabiki wa ngumi za kulipwa wataona kitu tofauti kabisa katika mchezo huo, " alisema Twisa.
Alisema kuwa kampuni yao chini ya udhamini wa Azam TV na Asas ina uzoefu mkubwa katika kuandaa matamasha, masoko na shughuli mbalimbali na kuahidi kufanya jambo la kihistoria hapa nchini.
"Tunataka kuona mabondia wanaendelea kwa kupata mapambano mengi ya ngumi na kinacho endana na kazi yao, tulifanya kazi na Mwakinyo kwa miaka mitatu na kuona ufanisi wake, tumeamua kuendelea naye na mabondia wengine wa Tanzania, tutaubadili mchezo wa ngumi nchini," alisema.
Kwa upande wake, Mwakinyo alisema kuwa hiyo ni fursa kwake na kuahidi kufanya vyema siku hiyo.
"Namshukuru Twisa na kampuni ya Jackson Group Sports ambao wameonyesha nia ya kuubadili mchezo wa ngumi za kulipwa, sitawaangusha watanzania," alisema Mwakinyo.
Mwakilishi wa WBF nchini Tanzania, Chatta Michael alisema kuwa rais wa shirikisho hilo, Goldberg Howard atasimamia mapambano hayo.