DAR: WAKATI zikiwa zimebaki siku 25 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu, upepo wa kisiasa kwa mgombea urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe umemwendea kombo, baada ya viongozi wa chama hicho, kutangaza kumuunga mkono Lissu, IJUMAA linachambua.
Hatua hiyo imetafsiriwa na wachambuzi wa kisiasa kuwa, zimwi la Edward Lowassa aliyekuwa mgombea wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, ndilo lililomtafuna Membe na kummaliza kisiasa, licha ya kuja na nguvu pamoja na ari kubwa kwa malengo ya kumtikisa Dk. John Magufuli.
Membe na Lowassa ambao wamekuwa na safari yenye mfanano kisiasa, wote walikuwa na ndoto ya urais ambao umeyeyuka mithili ya barafu juani, baada ya kila mmoja kushindwa kuhimili mikiki ya upinzani.
Hata hivyo, Lowassa anatajwa kuwa na mafanikio zaidi, kutokana na ujio wake upinzani baada ya kuuwezesha kupata wabunge 116 katika uchaguzi huo wa 2015, lakini Membe mbinu zake zimeonekana kufeli hata kabla ya kufikia sanduku la kura Oktoba 28 mwaka huu.
Safari ya Membe
Membe ambaye amekuwa na ndoto ya kuwa Rais wa Tanzania kwa takribani miaka kumi sasa, alichukua fomu ya kutaka kupitishwa na CCM kuwania urais mwaka 2015, kabla ya kukwaa kigingi na Dk. Magufuli kupeta.
Hata hivyo, kutokana na wasifu wake kama mbunge kwa takriban miaka 15, waziri kwa takriban miaka kumi, Membe alirejea kwa ujasiri wa kukemea maovu hata wakati akiwa ndani ya CCM katika kipindi cha uongozi wa Dk. Magufuli, jambo ambalo lilimzidishia anguko lake ndani ya chama hicho.
Kutokana na hali hiyo, Juni mwaka huu alitimuliwa ndani ya CCM na kuhamia ACT Wazalendo ambako aliteuliwa kuwa mgombea urais.
Licha ya kupewa nafasi hiyo adimu, katika wiki mbili za kampeni zake, mdororo mkubwa ulijitokeza katika nyanja mbalimbali ikiwamo maandalizi hafifu, uhaba wa wahudhuriaji kwenye mikutano yake, jambo ambalo linatajwa kumkimbiza na kuelekea Dubai alikodai kwenda kucheki afya yake, huku akisitisha kampeni zake kwa zaidi ya wiki tatu sasa.
Aidha, wakati kampeni zikipamba moto, Mwenyekiti wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamadi, alitangaza kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu, ikiwa ni siku chache baada ya Lissu kutangaza kumuunga mkono Maalim kuwa mgombea urais huko Visiwani Zanzibar.
Hatua hiyo inatajwa kusababishwa na mambo kadhaa, ambayo wachambuzi wa siasa wanaona yamekuwa kihunzi kwa Membe kinachomlazimu kufikia tamati ya safari yake kisiasa.
MZIMU WA LOWASSA
Dk. George Kahangwa alisema ni dhahiri kuwa, mzimu wa Lowassa ni mojawapo ya Membe kukwama katika siasa za upinzani.
Dk. Kahangwa alisema, ujio wa Membe upinzani licha ya kwamba bado hajarejea CCM, unashabihiana na safari ya Lowassa kuelekea Chadema na kurudi CCM.
Alisema hali hiyo imesababisha wananchi kutowaamini wakongwe, wanaotoka CCM kuja upinzani kusaka madaraka kama alivyofanya Membe.
“Kwa sababu Membe ndoto yake ni kuwa rais, hakuna kingine, vivyo hivyo kwa Lowassa, lakini Lowassa alifanikiwa kidogo tofauti na Membe, ambaye amekata tamaa mapema na hata viongozi wake kushindwa kuvumilia,” alisema.
LISSU ALIVYOKWAPUA NYOTA YA MEMBE
Hatua ya Membe kujiunga na ACT Wazalendo miezi miwili iliyopita, ilizimua siasa za upinzani hapa nchini kwa sababu wakati huo, hakukuwa na uhakika endapo Lissu angerejea nchini na kuwania urais kama alivyokuwa ametangaza.
Upinzani ulikuwa unalilia kuwa na mgombea wa kushindana na Rais Magufuli na kigogo huyo aliyefukuzwa kutoka katika chama chake, alikuwa na sifa zote za kuwa kinara wa upinzani.
Watu wengi walidhani Lissu hatarejea kwa sababu za kiafya kutokana na shambulio dhidi yake, lililofanywa Septemba mwaka 2017 au kwa sababu tu ya uoga wa kukamatwa kwa sababu yoyote ile.
Rais huyo mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika na mbunge, alikuwa hajarejea nchini tangu mwaka 2017 na wapo walioamini kuwa, kuna nafasi ndogo sana kwake kurejea nchini.
Hata hivyo, kurejea kwake, kuliamsha ari na muamko wa shamrashamra za kisiasa nchini, kiasi cha Lissu kumzima kabisa Membe.
Mchambuzi wa siasa Mselemu Lino kutoka chuo kikuu cha Ruaha, alisema Watanzania wengi walikuwa na shauku ya kumuona Lissu kuliko Membe, ndiyo maana kampeni za ACT Wazalendo Bara, zikadorora ghafla.
ATAKUBALI KUCHUTAMA?
Baada ya Maalim Seif kutangaza kumuunga mkono Lissu urais Bara, wengi wanasubiri kauli ya Membe kukubaliana na viongozi wake.
Hatua hiyo inatokana na ukweli kuwa, tayari Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe ameweka wazi kuwa kesho Oktoba 3, wanatarajia kutangaza hatima ya ushirikiano wao na Chadema.
Matarajio makubwa ni kushirikiana baina ya vyama hivyo viwili, hasa baada ya Lissu naye kutangaza kuwa, Chadema inamuunga mkono Zitto katika jimbo la Kigoma Mjini.
Kutokana na mazingira hayo, macho na masikio ya Watanzania, yanabaki kumsubiri Membe iwapo atakubali kuzima ndoto yake ya urais mwaka huu.
NDIYO MWISHO WAKE KISIASA
Aidha, Profesa Gaudence Mpangala kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha, anasema safari ya Membe kisiasa, ni dhahiri kuwa sasa imefikia tamati.
Alisema iwapo ACT Wazalendo wakimuunga mkono Lissu rasmi katika safari yake ya urais, ina maana Membe atakuwa ameenguliwa na kuwekwa kando kwa sababu mazingira yanaonesha kuwa, Membe hataki kukubali maamuzi hayo.
Alisema kwa kuwa Membe tayari kashindwa kukubali upinzani, na upande wa CCM alikotoka alifukuzwa, ina maana kuwa atalazimika kuandika barua ya kuomba msahama ili arejeshwe ndani ya CCM.
“Kwa mazingira hayo, itategemea na utashi wake kisiasa kwa sababu tayari umri umeenda, na hana cha kupoteza tena kwenye siasa, hatuwezi kumtafsiri kama atakuwa na nguvu kubwa tena mwaka 2025, kwa sababu kutakuwepo na chipukizi wapya hususani vijana, ambapo 2020 amedhihirisha kushindwa kuwashawishi,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa tayari Membe alistaafu kugombea ubunge mwaka 2015, atabaki kusubiri huruma kupitia teuzi za Rais atakayekuwa madarakani, iwapo atabaki ACT Wazalendo na Lissu akashinda au akirejea CCM na Dk. Magufuli akafanikiwa kuendelea.