KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uweneziwa Chama cha Mapinduzi CCM, Humphery Polepole amesema kwamba chama cha Mapinduzi CCM kimetoa maelekezo kwa wagombea wake wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na visiwani Zanzibar kujikita zaidi katika kunadi sera pamoja na muelekeo wa nchi endapo watachaguliwa na wananchi.
Polepole amesema kuwa CCM kwa sasa wanajikita zaidi katika kuwaonesha watanzania wapi nchi inapoelekea ila wapinzani wao wanadi sera za uongo pamoja na kujikita katika kupotosha watanzania.
Hayo amayaeleza leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu uliofanyika ofisi kuu za Chama cha Mapinduzi CCM, Zanzibar, Kisiwandui Mjini Unguja.
Polepole alisema, Chama cha Mapinduzi CCM kwa hiari yake imeamua kutoa maagizo wa wagombea wao kujikita zaidi kutangaza muelekeo wa nchi wanapotaka kuifikisha.
"Tumewaambia watangaze sera na muelekeo wa Taifa tunapotaka kulifikisha na si kutangaza tulichokifanya hapo nyuma maana watanzania tayari wameshayaona maendeleo makubwa yaliyofanywa na Chama cha Mapinduzi CCM," alisema Polepole.
Aliongeza kusema kwamba Wagombea wote ambao ni Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Dk. Hussein Ali Mwinyi wajikite katika kutangaza maono ya nchi wanapotaka kuifikisha pamoja na kutangaza maono yalikuwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020/2030.
"Mbali na kutangaza maono yao, wajikite zaidi katika kutangaza muelekeo wa Ilani ya chama cha Mapinduzi CCM 2020/2030 huko kuna kila kitu ambacho kinaonesha wapi ambapo CCM inataka kuifanyia nchi hii," alisema Polepole
Alifafanua kuwa tayari Dk. Magufuli na Dk.Mwinyi pamoja na viongozi wengine kama vile Kassimu majaliwa pamoja na Samia suluhu Hassani wameshapita kutangaza muelekeo wa chama hicho.
Katika hatua nyingine Polepole alisema kwamba chama cha Mapinduzi CCM kinaendelea na kampeni zake kama ratiba zilivyopangwa ambapo hadi sasa tayari makundi mbalimbali tumeshafikia kwa lengo la kunadi sera zao.
"Kwa upande wa Zanzibar na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wagombea wetu wameshawafikia makundi hayo na wanaendelea na Kampeni zao"alisema Polepole.