MWANAMUZIKI Rihanna ameomba msamaha kwa kutumia Hadith ya Kiislamu kwenye onyesho la nguo za ndani za kampuni yake ya Fenty. Alianza kukosolewa vibaya mtandaoni kwa kutumia wimbo unaojulikana kama Doom wa msanii Coucou Chloe, ambao unajumuisha maudhui ya Kiislamu yanayofahamika kama Hadith.
Rihanna amesema utumiaji wa nyimbo hiyo ulikuwa “ukosefu wa umakini.” Hadith ni sehemu ya baadhi ya maneno ambayo yanaaminika kuzungumzwa na mtume Muhammad.
Baada ya kitabu kitakatifu cha Quran, Hadithi inachukuliwa kuwa baadhi ya maneno muhimu kwenye dini ya Kiislamu. Mashairi ya Kiarabu ya wimbo huo ni sehemu ya Hadith kuhusu siku ya kiyama. Baadhi ya wafuasi wake wa Kiislamu walianza kuhoji matumizi ya wimbo huo kwenye onyesho lake lililonyeshwa moja kwa moja kupitia mtandao wa Amazon Oktoba 2.
Aidha, Coucou Chloe pia ameomba msamaha na kusema hakujua kwamba wimbo huo una mashairi ya dini ya Kiislamu. Lakini hii siyo mara ya kwanza Rihanna kushutumiwa kwa kufanya mambo yasiokubalika na yanayolenga dini ya Kiislamu. Mwaka 2013, aliombwa kuondoka katika msikiti mmoja huko Adu Dhabi baada ya kuonekana akipiga picha zisizofaa.