Zikiwa zimepita siku 11, tangu mrembo Wema Sepetu kuzua gumzo kwa kukiri kudanganya umri, hatimaye Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limeanza kufuatilia jambo hilo.
Septemba 28, mwaka huu, kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram akiwa anasheherekea siku yake ya kuzaliwa, Wema aliweka picha aliyokuwa amevaa gauni jekundu na kujipongeza kwa kufikisha miaka 30.
Katika picha hiyo ilisindikizwa na maelezo yaliyosema: “Miaka 30 malaika, niliahidi kusema ukweli kuhusu siku yangu. Septemba 28 mwaka 1990 nilitoka tumboni mwa mama yangu Mariam Athuman Sumbe, nina furaha kusheherekea miaka 30 ya maisha yangu, samahani nilidanganya.”
Maneno hayo ya Wema yalipokewa kwa mitazamo tofauti na watu, huku baadhi wakionekana kukerwa na tabia ya baadhi ya wasanii kudanganya umri wao.
Pia wafuatiliaji wa masuala ya urembo walimpigia hesabu ya umri aliokuwa nao mwaka 2006 aliposhiriki mashindano ya Miss Tanzania alipotwaa taji la mashindano hayo, ambapo ilionekana kuwa alikuwa na miaka 16 tofauti na 19 aliyejitambulisha wakati huo.
Kutokana na hilo, Mwanaspoti lilizitafuta mamlaka husika ikiwemo Basata kutaka kujua namna walivyochukulia suala hilo, ambapo katibu wake, Godfrey Mngereza aliahidi kulifuatilia atakaporejea Dar es Salaam kwa kuwa siku hiyo alikuwa safari ya kikazi jijini Dodoma.
“Suala la umri wa Wema tayari tumeshaanza kulifanyia kazi ikiwemo kumuita kwa ajili ya kumhoji, na kwa sababu inahusisha na mamlaka nyingine kuthibitisha umri wa mtu (akimaanisha Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo- Rita), tayari tumeshawasiliana nayo, wanaifanyia kazi, hapo baadaye mtapata majibu ni hatua gani zitachukuliwa baada ya hapo ila kwa sasa lipo kiofisi zaidi,” alisema Mngereza.
Rita ambao ndio watoaji wa vyeti vya kuzaliwa walipotafutwa kupitia meneja Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Josephat Kimaro alisema bado hajapata taarifa kuhusiana na suala hilo.
“Unajua kuna idara nyingi pale ofisini za kuwasilisha malalamiko kuhusiana na masuala ya vyeti vya kuzaliwa na pia zipo njia nyingi za uwasilishaji, hivyo ishu ya Wema binafsi haijanifikia, ila naomba unipe muda niifuatilie na unitafute Jumatatu wiki ijayo nitakuwa katika sehemu nzuri ya kuizungumzia baada ya kujidhihirisha kwa wahusika wanaoshughulikia hayo mambo,” alisema.
Wakati Wema akikiri kudanganya umri, kisheria ili mtu ashiriki mashindano ya Miss Tanzania anapaswa kuwa na umri kuanzia miaka 18 hadi 23.