Serikali Yashinda Kesi Kupinga Muungano wa Tanzania

 


Mahakama ya Jumuiya Afrika Mashariki imetupilia mbali madai ya kupinga uhalali wa Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofunguliwa na baadhi ya wanaharakati.

 Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata ameeleza kuwa mahakama hiyo imetoa uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja zote za upande wa Serikali ikiwa ni pamoja na madai kuletwa nje ya muda, pamoja na uhalali wa mahakama kuhoji uhalali wa muungano huo.

Amesema Mahakama ya Afrika Mashariki imezaliwa kupitia makubaliano (The East African Community Treaty) ya mwaka 1999 na kuanza kufanya kazi mwaka 200, hivyo mahakama hiyo haina mamlaka ya kuhoji Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964.
 
--------------
 

OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU USIKILIZWAJI NA UAMUZI WA SHAURI NAMBA 09/2016 KATIKA MAHAKAMA YA HAKI YA AFRIKA MASHARIKI BAINA YA RASHID SALUM ADIY NA WENZAKE 39,999 DHIDI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, KATIBU MKUU KIONGOZI WA BARAZA LA MAPINDUZI LA ZANZIBAR NA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI, TAREHE 29/9/2020 SAA 3:30 ASUBUHI

  1. UTANGULIZI
    • Mnamo tarehe 02 Novemba 2016, Bw. Rashid Salum Adily na wenzake 39,999 walikwenda kwenye Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na kufungua Shauri Namba 09 ya Mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi la Zanzibar wakihoji na kupinga uhalali wa vifungu na Hati ya makubaliano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa sababu zifuatazo:-
  • Hati ya Makubaliano inayodaiwa kusainiwa tarehe 26/4/1964 baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar haipo (non existent)
  • Hati ya Makubaliano inayodaiwa kusainiwa tarehe 26/4/1964 baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar ni batili
  • Hati ya Makubaliano inayodaiwa kusainiwa tarehe 26/4/1964 baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar haijawahi kuridhiwa wakati wowote ule na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
  • Uwepo wa Jamhuri ya Muungano ni batili kwa sababu umetokana na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambao haujawahi ridhiwa na pande zote mbili za Muungano
  • Zanzibar ni Taifa huru na linalojitegemea kwani halijawahi ungana na Taifa lolote.
  • Hivyo, waliiomba Mahakama itoe tamko la kubatilisha Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao umetokana na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar.
  • Kwa upande wa Serikali ambao ni wajibu maombi, waliwasilisha majibu ya Utetezi juu ya Uhalali wa kisheria wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja mapingamizi ya awali ya kisheria. Mapingamizi hayo ni;
  • Kwamba, Mahakama ya Afrika Mashariki haina mamlaka kisheria  kusikiliza hoja za kupinga uwepo wa Taifa la Tanzania lililotokana na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar,
  • Kwamba, madai yamewasilishwa nje ya muda uliowekwa na Ibara ya 30(2) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 1999.
  1. USIKILIZWAJI WA SHAURI
    • Shauri lilisikilizwa tarehe tarehe 6/7/2020 kwa njia ya Video ( Video Conference) ambapo wadai waliwakilishwa na Mawakili wa Serikali kutoka  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wa Tanzania pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar ambao ni;
  1. Gabriel P. Malata- Wakili Mkuu wa Serikali
  2. Vicent Tango-Wakili wa Serikali Mkuu
  3. Ali. A. Hassan-Wakili wa Serikali Mkuu
  4. Juma Msafiri-Wakili wa Serikali Mkuu
  5. Mbarouk Othman Suleiman-Wakili wa Serikali Mwandamizi
  6. Stanley Kalokola-Wakili wa Serikali
  • Upande wa Walalamikaji uliwakilishwa na Wakili Rashid Mutola

 

  • HOJA ZA SERIKALI KATIKA MAPINGAMIZI YA AWALI :
  • Serikali ilipinga uwezo wa Mahakama kusikiliza Shauri linalohusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa hoja zifuatazo
  • kwa mujibu wa Ibara ya 27 na 30 ya Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mhakama haina mamlaka kisheria kuhoji uhalali na uundwaji wa nchi yoyote ile kwani kufanya hivyo ni sawa na hata mahakama yenyewe kujihoji kuhusu uhalali wake kwani umetokana na uwepo wa nchi hizo zinazounda jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwemo na Hoja ya msingi katika ibara tajwa ni kwamba Mahakama haina mamlaka ya kuhoji Muungano huo na kwa kwamba hoja za walalamikaji hazina mashiko mbele ya Mahakama hiyo.
  • Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza na kutafsiri vitendo, maamuzi yaliyofanywa na Taifa huru kabla ya kuanzishwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki na Taasisi zake ikiwemo Mahakama yenyewe
  • Madai yameletwa nje ya muda wa siku sitini(60) kama inavyoelekezwa na ibara ya 30(2) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

  • HOJA ZA WALALAMIKAJI KUHUSU MAPINGAMIZI YA AWALI.
  • Walalamikaji kupitia Bw. Rashid Mutola walipinga hoja za Serikali kwa hoja kwamba Mahakama ina mamlaka na malalamiko ya wateja wake yanahusu haki za binadamu kwani wakati wa kuanzishwa Muungano wananchi wa Zanzibar hawakushirikishwa. Aidha, walalamikaji walidai kwamba madai yao ni ya msingi.
  • Na hivyo waliomba mapingamizi ya Serikali yatupiliwe mbali na shauri liendelee kusikilizwa kwa wahusika kuendelea kutoa ushahidi kama ilivyokubaliwa kwenye Kongamano la pamoja (scheduling conference).


  • UAMUZI WA MAHAKAMA:

Shauri hili limetolewa uamuzi tarehe 29/9/2020 kwa njia ya Video (Video Conference). Katika Maamuzi yake, Mahakama imekubaliana na hoja zote za Serikali kuhusu kutokuwa na uhalali wa kisheria wa Mahakama kusikiliza Shauri hilo. Pamoja na mambo mengine, Mahakama imekubaliana na hoja zote za Serikali. Katika uamuzi wake Mahakama ilieleza mambo yafuatayo:-

  • Mahakama haina mamlaka ya kisheria kuhoji uwepo Taifa huru wa Jamhuri ya Muungano Tanzania ikiwa ni pamoja kutoka tafsiri ya maamuzi ya nchi mbili huru zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanganyika na Zanzibar sio nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki
  • Mahakama imekubaliana na hoja kwamba, wadai hawana hoja yoyote dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani wadai wameshindwa kuthibitisha madai yao kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo wakati Hati za Muungano zinasajiliwa katika Umoja wa Mataifa na kutambuliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna mapingamizi yaliyowasilishwa kupinga hati za Muungano kutoka kwa Tanganyika au Zanzibar.
  • Mahakama pia ilikubaliana na hoja madai yaliwasilishwa nje ya siku 60 zinazotajwa katika ibara ya 30(2) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
  • Kuhusu gharama, Mahakama imeamua kila upande ubebe gharama zake kwa kuzingatia kwamba shauri hilo liliwasilishwa kwa kuzingatia maslahi ya Umma (public interest).
  • Mwisho, Shauri hili limetupiliwa mbali kwa hoja zilizotajwa hapo juu.

Imeandaliwa na

Gabriel Pascal Malata,

Wakili Mkuu wa Serikali,

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali,

Dar es Salaam, 30 Septemba 2020.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad