Shelisheli Inavyoipa DUNIA Tuition ya Kisiasa

 


OKTOBA 22, mwaka huu, Shelisheli walianza kufanya uchaguzi wa Rais. Walikamilisha Oktoba 24 (juzi). Kiongozi wa chama cha Seychelles Democratic Alliance, Wavel Ramkalawan, ameshinda.


Ramkalawan, mchungaji wa Anglican, amemshinda Rais Danny Faure. Kabla ya ushindi huo, Father Ramkalawan alishagombea urais wa Shelisheli mara sita bila mafanikio. Ya saba kashinda.


Shelisheli ilipata uhuru mwaka 1977, ikawa chini ya mfumo wa chama kimoja. Mwaka 1993 ilikaribisha mfumo wa vyama vingi. Wakati huo wote, chama tawala cha United People’s Party ambacho sasa kinaitwa United Seychelles Party, kikawa kinashinda. Safari hii imekuwa mara ya kwanza kwa chama cha upinzani kushinda mamlaka ya Serikali Shelisheli tangu uhuru.


TUITION YA SHELISHELI


Baada ya matokeo kutangazwa, Father Ramkalawan na Rais Faure, walitokeza mbele ya vyombo vya habari pamoja.


Ramkalawan akasema: “Mimi na Faure ni marafiki wa karibu. Uchaguzi sio mwisho wa mchango wa kila mmoja kwenye nchi yake. Katika uchaguzi huu hatukuwa na mshindi wala mshindwa. Mshindi wa jumla wa uchaguzi huu ni nchi yetu, Shelisheli.” Wakati Father Ramkalawan akisema hayo, Rais Faure alikuwa akitikisa kichwa kuonesha kukubaliana na kilichosemwa.


Kipindi hiki ambacho dunia ipo kwenye harakati za uchaguzi katika nchi nyingi, tunashuhudia visa vya chuki na siasa za kung’ang’ania madaraka, Faure na Ramkalawan wanaionesha dunia kwamba uchaguzi ni kwa ajili ya nchi. Kukubali matokeo inawezekana. Mshindi na mshindwa wanaweza kupeana mikono kwa upendo.


Kipidi hiki Guinea na Ivory Coast wanahesabu idadi ya watu waliopoteza maisha kisa uchaguzi. Rais Donald Trump akigoma kutamka kuwa akishindwa uchaguzi ataachia madaraka. Rais Faure na Father Ramkalawan wanaipa somo kubwa dunia.


Faure na Ramkalawan ni somo pia kwa Tanzania. Tunakwenda kwenye uchaguzi Keshokutwa (Oktoba 28). Yapo mazingira na zipo kauli tata. Tanzania ni nchi kubwa. Tunahitaji siasa za heshima, zenye utii wa demokrasia. Wananchi ndio waamue kesho yao. Jukumu la wanasiasa ni kuheshimu uamuzi wa wananchi.


Uchaguzi wa Tanzania si wa tume, polisi wala jumuiya ya kimataifa. Ni wa Watanzania.


Ndimi Luqman MALOTO

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad