Michezo miwili ya ligi kuu soka Tanzani bara raundi ya 7 itachezwa jioni ya leo Oktoba 22, 2020, jijini Dar es salaam na mkoani Rukwa.
Timu ya wananchi Yanga SC, watakuwa wenyeji wa Polisi Tanzania mchezo utakaochezwa uwanja wa Uhuru Dar es salaam, katika mchezo huu tutamshuhudia kocha mpya wa Yanga Cedric Kaze, akikiongoza kikosi hicho cha mabingwa wa kihistoria katika mchezo wake wa kwanza akiwa kama kocha mkuu.
Kwenye mechi mbili za ligi kuu walizokutana msimu uliopita, michezo yote ilimalizika kwa sare ikiwemo sare ya bao 3-3, katika mchezo uliochezwa uwanja wa Uhuru Dar es salaam na ule ulichezwa Ushirika Moshi ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Yanga haijapoteza mchezo hata 1 katika michezo 5 ya ligi, wameshinda michezo 4 na wamepata sare mchezo 1, na wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa na mfululizo wa kushinda michezo 4. Kikosi cha Polisi chini ya kocha Malale Hamsini kimepoteza mchezo 1 tu na wameshinda michezo 3 na wametoka sare michezo 2 kwenye michezo 6 ya ligi kuu.
Tofauti ni alama 2 kati ya timu hizo kwenye msimamo wa ligi, lakini Polisi wamecheza mchezo 1 zaidi ya Yanga kikosi hicho kipo nafasi ya 7 na alama 11, katika michezo 6. Kikosi cha Yanga kimekusanya alama 13 kwenye michezo 5 na wanashika nafasi ya 3 kwenye msimamo.
Huko mkoani Rukwa mabingwa watetezi Simba SC, wapo ugenini kuminyana na wenyeji wao Tanzania Prisons katika Dimba la Nelson Mandela.
Tanzania Prisons wanaingia katika mchezo wa jioni ya leo wakiwa hawajashinda mchezo hata 1 katika michezo yao 3 iliyopita, wamefungwa mchezo 1 na sare michezo 2, kikosi hicho cha maafande wa magereza kimeshinda mchezo 1 tu wa ligi kuu msimu huu katika michezo 6 waliocheza mpaka sasa. Wanaalma 6 na wapo nafasi ya 14 kwenye msimamo.
Simba wameshinda michezo yao yote mitatu iliyopita, lakini pia hawajapoteza mchezo ugenini msimu huu wameshinda michezo 2 na sare mchezo 1 katika michezo 3 waliocheza ugenini.
Mpaka sasa kikosi hicho cha mabingwa watetezi kimekusanya jumla ya alama 13 na kipo nafasi ya 2 kwenye msimamo wa ligi. Msimu uliopita katika michezo yote ya ligi waliyokutana ilimalizika kwa suluhu