HATIMAYE Klabu ya Simba imeanza kuichunguza Yanga kuanzia ilipopata kocha mpya Cedric Kaze.Yanga ambayo imejifungia Kigamboni jijini Dar es Salaam, imekuwa ikifanya mazoezi kwa siku mara mbili, asubuhi na jioni ndani ya ulinzi mkali.
Hata hivyo, awali Simba hawakuwa na presha kubwa na Yanga kwa kuwa kikosi chao kilionekana kutokuwa imara sana lakini baada ya kumpata kocha mpya upepo umeonekana kubadilika.
Chanzo cha ndani kutoka Simba, kimelieleza Championi Jumatano kuwa timu hiyo imekuwa ikifanya juhudi kubwa sana kuhakikisha kuwa inapata video za mazoezi ya Yanga ili kufahamu mbinu za wapinzani wao hao.
“Bado tunajiandaa na mechi zetu lakini kama unavyofahamu sasa ushindani umekuwa mgumu sana kwa kuwa Yanga wanaonekana kuwa siriazi kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu.
“Unajua kocha wao aliyeondoka (Zlatko Krmpotic), hakuwa na mazoezi magumu sana wala ya mbinu, lakini sasa inaonekana kuwa kuna jambo la tofauti, kuna watu wanataka kuona hata video za mazoezi yao, lakini imekuwa ngumu kwa kuwa wana ulinzi mkali sana kule Kigamboni.
“Lakini kwa kuwa wapo hapa Dar basi naamini kuna watu watafanya kazi hiyo kwenye mchezo wao wa keshokutwa (kesho) kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam wakati wakicheza na Polisi Tanzania na watamueleza kocha kile walichokiona.
“Labda hii ndiyo itakuwa nafasi yetu ya kufahamu kuwa wamebadilika kwa kiwango gani kabla hatujakwenda kwenye michezo mingine na baadaye mchezo wetu wa Novemba 7.
“Tunachofahamu tu mpaka sasa ndani ya siku tatu ni kwamba kocha wao anaweka mkazo kwenye safu ya ushambuliaji lakini bado hutajapata moja kwa moja anatumia staili gani,” kilisema chanzo hicho.
Yanga wanashika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 13 baada ya kucheza michezo mitano, wameshinda minne na kutoka sare mmoja.Simba wao wapo nafasi ya pili wakiwa wamepata matokeo sawa na Yanga lakini wakiwa na tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam