Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi, (CCM), Dkt. John Magufuli, amesema kuwa anatamani Taifa la Tanzania liendelee kuheshimika zaidi duniani na kwamba anatamani siku moja Tanzania iingie uchumi wa kwanza.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 26, 2020, wakati akizungumza na wananchi wa Dodoma, ikiwa ni muendelezo wa mikutano yake ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika siku ya Jumatano ya Oktoba, 28 mwaka huu.
"Natamani Taifa hili liwe Taifa linaloheshimika duniani na wameanza kutuheshimu baada ya kutokea Corona, sisi tukaizima kwa jina la Mungu wengine bado wanateseka, nina uhakika katika kipindi cha miaka mitano tumetoka kwenye dimbwi la kuitwa nchi maskini, tukaingia uchumi wa kati, tunataka siku moja nchi hii iwe kwenye uchumi wa kwanza katikati hatutaki", amesema Dkt Magufuli.
Awali Dkt Magufuli akiwa katika jimbo la Kondoa akiomba kura alisema maneno haya, "Hamchagui Malaika mnachagua binadamu ninawaomba ndugu zangu ili mnisaidie kupata 'Connection' ya kazi, nipate watu watakaokuja ofisini aniambie CCM oyee!, mheshimiwa kwenye ilani ya uchaguzi umesahahu hiki kwa ajili ya Kondoa".