Rais wa Marekani, Donald Trump aliondoka kwa muda mfupi jana katika hospitali ya kijeshi ya Walter Reed alikolazwa, kwa ajili ya kuwasalimu wafuasi wake waliokuwepo nje ya hospitali hiyo. Trump aliwapungia wafuasi hao akiwa kwenye msafara wa rais.
Madaktari wanaomtibu Trump wamesema kiongozi huyo anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali leo Jumatatu, iwapo ataendelea kupata nafuu kutokana na kuugua virusi vya corona.
Awali Trump aliweka ujumbe wa video mtandaoni akiwashukuru madaktari na pia amesema amejifunza mambo mengi kuhusu ugonjwa wa COVID-19.
Mapema jana, daktari wa Ikulu ya Marekani, Sean Dooley alisema hali ya Trump inazidi kuimarika, lakini alipata dalili mbaya siku ya Ijumaa.
Amesema Trump alikuwa na homa kali na kiwango cha oksijeni katika sampuli ya damu kilikuwa chini ya asilimia 94, lakini aliwekewa oksijeni ya ziada kwa muda wa saa moja katika Ikulu ya White House.