MREMBO anayeuza nyago kwenye video za muziki (video queen) mwenye visa lukuki Bongo, Anna Sebastian Kimario ‘Tunda’ amesema kuwa ili uweze kukua kiakili hadi umri, lazima kukabiliana na changamoto mbalimbali hasa za kwenye mitandao ya kijamii.
Tunda au Cappuccino amefanya mahojiano ya ana kwa ana (exclusive) na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA na kuweza kufunguka vitu vingi kuhusu maisha yake ya sasa hivi na vitu vingi vinavyozungumzwa juu yake kwenye mitandao ya kijamii;
IJUMAA WIKIENDA: Vipi Tunda, habari za siku, unaendeleaje maana umekuwa kimya kwa muda mrefu tofauti na zamani? TUNDA: Nipo, unajua kuna wakati unapaswa kutulia na kutafakari mambo mengi yanavyoendelea na watu kusahau kidogo, maana kila kukicha wanapenda kukuzungumzia tu.
IJUMAA WIKIENDA: Nimeona hata akaunti yako kwenye Mtandao wa Instagram umeifanya kuwa ya biashara, ni wewe au ‘imehakiwa’ maana mastaa ni vigumu kufanya matangazo kwenye akaunti zao?
TUNDA: Hapana, kama kuna fursa kubwa ya kufanya matangazo kwenye akaunti yako kwa nini usiitumie? Maana hakuna sababu ya kukaa nayo tu, bila kukuingizia kitu chochote, zaidi watu wachunguze picha zako na kukuchamba tu na mwisho wa siku watu waidukue, nipate gharama tena ya kuirudisha? Hapana, bora niitumie kibiashara nipate chochote.
IJUMAA WIKIENDA: Pesa ya matangazo unayopata inaweza kukidhi mahitaji yako yote?
TUNDA: Kabisa; yaani sina tatizo lolote na huwezi kuamini, pesa ya matangazo nikiiweka vizuri na kuitunza, naweza hata kununua ndege; yaani sina tatizo lolote kama naweza kupata hata milioni tano kuna tatizo gani? Kingine mimi ni mtu wa kukubaliana na hali yoyote.
IJUMAA WIKIENDA: Kumekuwa na wimbi la mastaa wa kike mara nyingi wanagombana na kuwekana kwenye mitandano ya kijamii, lakini wewe umekuwa tofauti, ni kwa nini?
TUNDA: Mimi sijaumbwa hivyo na ninajua watu wanavyoniona kwenye mitandao ya kijamii wananichukulia tofauti, lakini sivyo nilivyo kwa sababu nimelelewa na wazazi wazuri ambao wamenifundisha maadili yote.
IJUMAA WIKIENDA: Kuna kipindi fulani ulionekana kama una mimba, lakini ikapotea, halafu ikasikika tena unayo, ikayayuka tena, nini hasa huwa kinatokea?
TUNDA: Jamani hata mimi naona watu wanazungumza hivyo, lakini ukweli ni kwamba sijawahi kuwa nayo; maana watu wa mitandao wana mambo sana. Lakini muda wangu ukifika tu nitakuwa nayo.
IJUMAA WIKIENDA: Ila kuna kipindi picha zako nyingi zilionesha una tumbo kubwa au ulikuwa unalitengeneza?
TUNDA: Mimi naona labda hizo picha zilikuwa zinatengenezwa maana mimi sijawahi kuwa na mimba, sema ndiyo hivyo watu wakikuamulia, wanafanya yao tu.
IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusu ndoa yako na mpenzi wako Whozu kwani mmekaa muda mrefu kama wapenzi?
TUNDA: Unajua unaweza kusema kitu, halafu huko mbeleni mambo yakaenda ndivyo sivyo, lakini ninachoamini mimi ndoa hupangwa na Mungu. IJUMAA WIKIENDA: Lakini malengo ni muhimu…
TUNDA: Hilo bado sitaki kuliweka waziwazi kwa sasa, lakini kikubwa ni kuombeana nina kwangu, ninaishi Mbezi (Beach, Dar). Nikienda hotelini ni kwa ajili tu ya kubadilisha mazingira na hata wengine wanaweza kufanya hivyo, lakini pia kwa nini kila kukicha mtu anafuatilia mambo ya watu, si jambo jema, lakini mimi nafurahia, waendelee tu kufikiria hivyohivyo kuhusu mimi.
IJUMAA WIKIENDA: Mara nyingi unaonekana ni mtu wa kula bata sana, tena viwanja vya bei mbaya mno, unapata wapi pesa za kufanya matanuzi au ndizo hizo za matangazo?
TUNDA: Unajua Bongo, watu wengi wanapenda mtu akiwa anafanya kitu lazima mitandao ijue, mimi nina ishu zangu zinaniingizia pesa na pia siwezi kuweka kila kitu kumuangalia, lakini hata ukiniangalia mimi sifanani kabisa.
IJUMAA WIKIENDA: Kuna ishu iliwahi kusikika kuwa mke wa mwanamuziki wa Uganda, Jose Chameleone aliwahi kutinga Bongo kukusaka kisa mume wake, vipi ishu hiyo ina ukweli wowote?
TUNDA: (kicheko) hiyo sipendi kuizungumzia kabisa.
IJUMAA WIKIENDA: Vipi kwa upande wa baba na mama yako wakiona kwenye mitandao unaandikwa kwa skendo inakuwaje?
TUNDA: Unajua wale ni wazazi wangu, wananijua vizuri mtoto wao, kwa hiyo wakisikia vitu tofauti hawawezi kunichukulia kwa hasira au kuvipokea moja kwa moja kwa vile wananijua.
IJUMAA WIKIENDA: Kuna kipindi ulikuwa umeamua kurudi shuleni, vipi umeshamaliza au unaendeleaje na masomo kwa sasa?
TUNDA: Ndiyo nilishamaliza ambacho nilikuwa ninasomea na ninaendelea na mambo mengine.
IJUMAA WIKIENDA: Ni kitu gani unachotamani kwa sasa? TUNDA: Yaani ninatamani siku Instagram ifungwe hata mara moja maana watu wote maisha yao ni kule na wanaweza kuyachambua maisha ya mtu kupitia kule kumbe wala siyo sehemu sahihi ya kumjua mtu alivyo.