UKUTA wa Klabu ya Yanga unaoongozwa na nahodha Lamine Moro pamoja na Bakari Mwamnyeto umeweka rekodi matata Bongo kwa kuwa ni namba moja kwa timu zote 18 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kufungwa mabao machache na kuongoza kwa kufunga mabao mengi.
Yanga ikiwa imecheza jumla ya mechi tano ambazo ni sawa na dakika 450, imeruhusu kufungwa bao moja pekee tofauti na ukuta wa vinara wa ligi ambao ni Azam FC wakiongozwa na beki bora wa msimu wa 2019/20, Nicolas Wadada ambao umeruhusu kufungwa mabao mawili baada ya kucheza mechi sita.
Mbali na Azam FC pia watani zao wa jadi, Simba chini ya Joash Onyango na Pascal Wawa safu yao ya ulinzi imeruhusu kufungwa mabao mawili ndani ya dakika 450.Kabla ya mechi za jana ni ukuta wa JKT Tanzania inayonolewa na Kocha Mkuu, Abdallah Mohamed ulikuwa umeruhusu mabao mengi ambayo ni tisa baada ya kucheza mechi sita.
Pia kwa upande wa beki kinara wa kufunga, anatoka Yanga ambaye ni Lamine Moro amefunga mabao mawili huku Kagera Sugar wakiwa naye David Luhende na Simba wakiwa naye Pascal Wawa wote wamefunga bao mojamoja
NA LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam