Katika mwendelezo wa matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kumeshuhudiwa sura mpya kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM),katika majimbo yaliyoonekana na kuaminika kuwa ni ngome za vyama vya upinzani ikiwemo chama kikuu cha upinzani CHADEMA
Miongoni mwa majimbo hayo ni pamoja na jimbo la Hai, Moshi Mjini, Mbeya Mjini, Arusha Mjini, Iringa Mjini, Ubungo, Tarime Mjini, Tarime Vijijini na Kawe.
Pengine mwanzoni ilikuwa vigumu kufikiria kuwa majimbo hayo yangetoka katika mikono ya vyama vya upinzani kwa wakati mmoja na katika uchaguzi mmoja lakini kwa sasa kama yupo aliyefikiria hivyo ni dhahiri kuwa wakati umepingana na fikra zake.
Je ngome hizo za upinzani kuwa chini ya CCM inamaanisha nini ? '' Maeneo hayo kupoteza ni kwa sababu Chama Cha Mapinduzi kimewekeza nguvu kubwa kwa maaana kwanza nguvu yenyewe ya Magufuli kama Rais wa Jamhuri ya Muungano, Amiri Jeshi Mkuu na msimamizi mkuu wa watumishi lakini jambo la pili unaweza kujiuliza suala dogo tu inawezekanaje CCM imeweza kushinda jimbo kama Hai alafu imeweza kushindwa Jimbo kama Mtwara Mjini kwa Hawa Ghasia kwa hiyo ni maswali ambayo yanakuwa na tafakuri nyingi sana'' amesema Mbwana Allyamtu, Mchambuzi wa Siasa za Kitaifa na Kimataifa.
Aidha Mbwana ameongeza kuwa '' Hatuwezi kusema kuwa ni ushindi wa CCM ila ni ushindi wa Dk. Magufuli kwa sababu katika kampeni zake amekuwa akihimiza mara nyingi kwamba anahitaji wabunge wa Chama Cha Mapinduzi ili aweze kuleta maendeleo''