Vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vyafikia mwisho



Vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyopiga marufuku kuiuzia au kununua silaha kutoka Iran vimefikia mwisho leo kama ilivyoafikiwa na madola yenye nguvu licha ya upinzani kutoka Marekani.


Umoja wa Mataifa uliipiga marufuku Iran kununua silaha ikiwemo vifaru na ndege za kivita kutoka mataifa ya kigeni mwaka 2010 kufuatia msuguano uliozuka kuhusiana na mradi wake tata wa nyuklia. Hapo kabla umoja huo uliweka vikwazo dhidi ya mauzo ya silaha kutoka Iran.


Ingawa yenyewe inasisitiza kuwa haina mipango ya kununua silaha, kwa nadharia lakini Iran sasa inaweza kununua silaha inazotaka kuimarisha hazina yake ya  zana na mifumo ya ulinzi ambayo imekuwepo tangu mapinduzi ya kiislamu yalipofanyika mwaka 1979. Pia nchi hiyo inaweza kuuza tena zana zote za kijeshi zinazotengenezwa na kampuni za ndani.


Jamhuri hiyo ya kiislamu imeitaja hatua ya kufikia mwisho kwa vikwazo vya silaha kama "siku ya ushindi kwa jumuiya ya kimataifa .. katika kupinga juhudi za utawala wa Marekani".


"Hatua ya leo ya kurekebisha ushirikiano wa ulinzi kati ya Iran na ulimwengu ni ushindi katika mwelekeo wa mshikamano wa dunia, amani na usalama kwenye kanda yetu" ameandika waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Mohamed Javad Zarif kupitia ukurasa wake wa Twitter.


Hata hivyo utawala wa Rais Donald Trump umesisitiza kuwa bado vikwazo dhidi ya Iran vinafanya kazi kwa kuwa yenyewe imetengua kipengele kimoja kutoka mkataba wa nyuklia kati ya Iran na madola yenye nguvu ambao Marekani ilijiondoa mwaka 2018. Madai hayo yamepuuzwa na jumuiya ya kimataifa.


Wakala unaoshughulikia ujasusi kwa ajili ya ulinzi nchini Marekani ulitabiri kuwa iwapo vikwazo dhidi ya Iran vitafikia mwisho, nchi hiyo itajaribu kununua ndege za kivita za Urusi chapa Su-30, Yak-130 kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi na vifaru aina ya T-90.


Kadhalika serikali mjini Tehran inaweza kujaribu kununua mfumo wa ulinzi wa makombora wa S-400 kutoka Urusi pamoja na mifumo ya ulinzi mahsusi kwa ajili ya maeneo ya pwani. China pia inaweza kuizuia silaha Iran.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad