Wafungwa 180 waliokuwa kifungoni wameripotiwa kuachiliwa huru mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Mali.
Kulingana na maelezo yaliyotolewa na afisa mmoja wa Mali, iliarifiwa kuwa wafungwa 70 waliachiliwa huru siku ya Jumamosi na wengine 110 siku ya Jumapili, ambapo walichukuliwa kutoka gereza la mji mkuu wa Bamako na kusafirishwa kusini mwa nchi.
Watu hao 180 waliokuwa wakidaiwa kuwa wanachama wa kundi la itikadi kali za kigaidi, wanasadikika kuachiliwa huru kwa matarajio ya kurejeshwa kwa kiongozi wa upinzani Soumaila Cisse aliyechukuliwa mateka mwezi Machi.
Mnamo tarehe 29 Machi wakati wa harakati za kampeni zikiendelea kabla ya uchaguzi mkuu, kiongozi wa chama cha upinzani cha URD Soumaila Cisse pamoja na wafuasi wake 11 walishambuliwa njiani walipokuwa wakielekea Koumaira kutoka Sarafere.
Walinzi wa Cisse waliuawa na wafuasi wake 2 wakajeruhiwa kwenye mashambulizi hayo.
Tangu siku hiyo hadi leo Cisse amekuwa akiishi kama mateka chini ya ulinzi wa washambuliaji.