Australia imeonesha kusikitishwa kwake na Qatar baada ya wanawake kuripotiwa kukaguliwa ndani ya maungo yao walipokuwa wakijaribu kuingia kwenye ndege kutoka Doha kuelekea Sydney.
Uchunguzi huo unaripotiwa kufanyika baada ya wafanyakazi katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamand kumkuta mtoto aliyezaliwa kabla ya muda wake bafuni.
Kuna ripoti mchanganyiko kuhusu kama mtoto alikuwa hai au alikuwa amekufa.
Raia 13 wa Australia ni miongoni mwa wanaoelezwa kuwa walifanyiwa uchunguzi.
Walibebwa kwenye gari la kubebea wagonjwa na kuambiwa wavue nguo zao za ndani kabla ya kuchunguzwa, Channel Seven iliripoti.
Wanawake hao hawakuambiwa kwanini walikuwa wakichunguzwa kabla ya kuingia kwenye ndege ya shirika la Qatar tarehe 2 mwezi Oktoba.
Serikali ya Australia imewasilisha suala hilo kwa mamlaka za Qatar.
''Tumewasilisha rasmi malalamiko yetu kuhusu tukio hilo kwa mamlaka za Qatar na tumehakikishiwa kupata taarifa za wazi na kina kuhusu tukio hilo muda mfupi ujao,'' msemaji wa wizara ya mambo ya nje na biashara aliwaambia wanahabari nchini Australia.