Wataalamu wa Afya waonya matumizi ya dawa za macho kiholela



Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Grace Maghembe,amesema inakadiriwa kuwa watanzania  laki sita hawaoni huku akitoa wito kwa wananchi kuepuka kutumia dawa ya macho kiholela bila ya kuwa na maelekezo kutoka kwa Daktari.


Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuadhimisha siku ya Afya ya macho Duniani Dkt.Maghembe amesema kuwa ni muhimu mtu kufika hospitalini mara tu anapoona kuwa ana matatizo ya macho na sio kutumia dawa ambazo sio rasmi kwa ajili ya matibabu 


 




Dkt Maghembe amesema inakadiriwa kuwa watanzania 600,000 hawaoni huku watu wenye matatizo ya kuona kwa kiwango cha kati na cha juu hapa nchini wanakadiriwa kuwa ni mara tatu ya watu wasioona ambao ni takriban milioni 1.8 hivyo kwa ujumla Tanzania ina watu milioni 24 wenye matatizo ya kuona .

“Watu milioni 24 sawa na asilimia 2.5 ya watanzania wote wana ulemavu wa kutokuona  ikijumuisha na upungufu wa kuona na asilimia kubwa ya  matatizo haya yanasababishwa na  upungufu  wa kuona unaorekebishika kwa miwani 45%,mtoto wa jicho 28.8%,shinikizo la jicho 8%, kovu kwenye kioo cha mbele cha jicho na Trakoma 5%, athari ya ugonjwa wa kisukari kwenye pazia la jicho na matatizo ya pazia la jicho kwa watu wazima 4%,matatizo ya kutokuona utotoni 2%,na Mengineyo 8.2%”amesema Dkt.Maghembe


Akizungumzia hali ya afya ya Macho na upungufu wa kuona Duniani Dkt.Maghembe amesema watu bilioni 1.1 duniani wana upungufu wa kuona vizuri ambapo wakati mwingine wangeweza kusoma ila sababu wamekosa miwani inayoweza kuwasaidia.


Pia,takriban watu milioni 253 duniani wanakadiriwa kuwa na upungufu wa kuona namna moja ama nyingine ambapo kati ya hawa milioni 36 wana ulemavu wa kutokuona kabisa  huku asilimia 89% ya watu wenye  upungufu wa kuona wanaishi katika nchi za uchumi wa chini na wa kati ikiwemo Tanzania.


Hata hivyo,Dkt.Maghembe amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya ulemavu wa kutokuona na upungufu wa kuona wa kati na wa juu unaweza kuepukika huku asilimia 55% ya watu wenye upungufu wa kuona wa kati na wa juu ni wanawake na tatizo la ulemvu wa kutokuona na upungufu wa kuona  limepungua na kufikia asilimia 2.7 kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 4.6% kwa mwaka 1990 ikiwa ni mafanikio ya azimio la Dira ya Haki ya Kuona   ifikapo mwaka 2020.


Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyo ya kuambikiza Dkt James Kiologwe amesema katika kuadhimisho siku hiyo wamejikita zaidi katika kutoa elimu ili kusaidia watu kuchukua hatua za kujikinga kupoteza uoni wa macho.


“Katika kuadhimisha siku hii muhimu tumejikita zaidi katika utoaji wa elimu ambapo tumekuwa tukiwafikia wadau katika kuhakikisha huduma za macho zinakuwa bora zaidi kwa kila mtu ambapo wapo watu 450 kati ya watu milioni moja wanapatiwa huduma za upasuaji wa macho lengo ni kufikia watu 2000 na pia kuhakikisha wanapona “amesema.


Kwa upande wake Rais wa Chama cha Madaktari wa Macho Tanzania Dkt Frank Sandi amesema ziko baadhi ya hospitali ambazo hazina madaktari wa macho hivyo kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbai ili kuona ni kwa jinsi gani kila mkoa unapata huduma za macho.


Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa ya Jijini Dodoma, Dk.Jasinta Feksi amesema kuwa mfumo wa hewa na moshi una athari kwa macho huku pia akibainisha kuwa miwani,jua ina madhara kwa macho ikiwa ni pamoja na kuota vinyama kwenye macho.


Akizungumza kwa niaba ya wadau wa Afya ya Macho Nesia Mahenge  kutoka Taasisi ya “CHRISTOFEEL BLINDEN MISSION[CBM]”amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa takwimu kwa watu wenye matatizo ya macho huku akibainisha kuwa wanaendelea kushirikiana na serikali  katika kuweka vipaumbele vya utatuzi wa changamoto ..


Maadhimisho ya siku ya Afya ya Macho Duniani kwa mwaka 2020 yamebeba kauli mbiu isemayo ‘’Afya ya Macho kwa wote ,Matumaini ya Kuona’’ ambapo kitaifa yamemeadhimishwa katika Mkoa wa Simiyu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad