STAA wa filamu nchini, Wema Sepetu amedaiwa kuitikisa ndoa ya mchezaji wa timu Yanga, Carlos Carlinhos ambaye ni raia wa Angola, baada ya mkewe Vanessa kutaka kuambiwa ukweli kuhusu picha aliyopiga Wema na mchezaji huyo, kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Mke wa mchezaji huyo ambaye, wamezaa mtoto mmoja wa kike, aliitupia picha kwenye mtandao wake wa Instagram na kuhoji kwa lugha ya kifaransa kuwa: “Nimetumiwa hii picha na mtu, nataka kujua kuna ukweli wowote,” aliandika huku akiwa amemtag mumewe kwenye Instagram.
Kutokana na watu wengi kutojua nini kimeandikwa na mke wa mchezaji huyo, wengi wao walifikiri kuwa anachukulia poa au anafurahia mumewe kupiga picha na staa huyo.
Baada ya gazeti hili kunyaka ubuyu huo, lilimnyanyulia waya, Wema, ambapo alipopewa taarifa hiyo alionekana wazi kushangaa na kutojua kama yamefika huko, hadi kwa mkewe kumaindi.
“Basi haya ni makubwa, mimi sijaona hii na hata kama ningeona nisingeelewa chochote, lakini pia sishtuki kwasababu sina uhusiano wowote na mumewe mimi, shauri yake!” alisema Wema.
Picha ya Wema na mchezaji huyo ilisambaa kwenye akaunti mbalimbali za udaku kupitia mtandao wa Instagram na Facebook huku watu wakiwa hawana majibu sahihi kuhusu ukaribu wa Wema na mchezaji huyo. Picha hiyo iliyoibua gumzo, inaonesha wawili hao walipiga picha kwenye duka la nguo la GSM, Mlimani City, jijini Dar.