BAADA ya Bodi ya Ligi Tanzania, (TBLB) kutangaza kuwa ule mchezo uliokuwa unasubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki wa soka nchini kati ya Yanga na Simba kupelekwa mbele, uongozi wa Yanga umesema kuwa ni jambo jema kwao kujiweka sawa zaidi.
Taarifa rasmi kutoka TPLB imeeleza kuwa sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kutokana na uwezekano wa wachezaji wa timu hizo mbili kuweza kupata vikwazo vya usafiri kutoka kwenye nchi zao jambo ambalo linaweza kuathiri vikosi vya timu hizo mbili.
Taarifa imefafanua kwamba kwa sasa nchi nyingi bado zinaendelea kuwa na vikwazo vingi kwenye masuala ya usafiri kutokana na janga la Virusi vya Corona kuendelea kusumbua nchi nyingi.
Ofisa uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema kuwa kwa kufanya hivyo kunatoa fursa kwa timu yao kujiandaa vema zaidi kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa Novemba 7.
Yanga tayari ilikuwa imeweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo na watani zao wa jadi Simba wanatarajia kuingia kambini, kesho kwa wachezaji ambao hawajaitwa timu ya Taifa.