Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema kuwa siku ya kupiga kura, atampigia kura mgombea urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu, kwa kuwa anamuamini sana na anayo dhamira ya dhati kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo Oktoba 16, 2020, na Kiongozi huyo na kusema kuwa chama hicho kimeshauriana na kuona kuwa kuna haja ya kuchagua kiongozi ambaye atarejesha furaha na kuheshimu katiba ya nchi.
"Kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi nitapiga kura yangu kwa ndugu Tundu Lissu, huyu ndiye mgombea wa upinzani ambaye ana nguvu ya kumshinda mgombea wa chama tawala, amefanya kampeni nchi nzima, mwitikio wa wananchi kwake ni mkubwa sana, ameeleza kwa ufasaha dhamira yake ya kuleta mabadiliko na sina mashaka na dhamira hiyo", amesema Lissu
Aidha Zitto amewaomba Watanzania kwa pamoja wampigie kura Lissu na kusema kuwa, "Sisi ACT Wazalendo hatupo tayari kuwa kizuizi cha safari hii ya mabadiliko, nami kama kiongozi wa chama ninao wajibu wa kulieleza hilo kwa uwazi kwa niaba ya viongozi wenzangu wa kamati ya uongozi''.
Mbali na hayo Zitto amewataka Watanzania kuwachagua wagombea wa ACT Wazalendo katika majimbo na wagombea wa upinzani wenye nguvu zaidi, huku yeye akitoa msimamo wake thabiti juu ya mgombea gani atakayempigia kura.
Awali Chama cha ACT-Wazalendo kilimteua Benard Membe ambaye alipitishwa na Tume ya Uchaguzi kuwania kinyang'anyiro cha urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.