Yaliyomo kwenye ziwa hilo kisayansi yanalifanya liwe ama hatari au lenye manufaa kwa mamilioni ya wakaazi walio karibu.
Ziwa la Kivu haliko kama maziwa mingine yenye kina kirefu.
Kawaida maji ya juu ya ziwa yakiwa baridi - kwasababu ya hali joto ya baridi au mito inayobeba theluji iliyoyeyuka, kwa mfano, - maji hayo baridi ambayo ni mazito huzama na yale ambayo sio mazito hupanda juu ya ziwa.
Mchakato huo kawaida hufanya eneo la juu la ziwa la kina kirefu kuwa na joto kuliko eneo la ndani.
Lakini kwa ziwa Kivu hali ni tofauti na kulifanya kuwa na matokeo ya ajabu.
Ziwa hilo likiwa limetapakaa hadi katika mpaka wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ni moja ya maziwa katika eneo la Bonde la Ufa la Afrika Mashariki ambako bara la Afrika linaachana na kugawanyika kwasababu ya nguvu za miamba.
Matokeo yake kunasababisha shughuli za volkeno mfano chemichemi za maji moto chini ya ziwa Kivu ambako kunakotoa maji moto, pia kuna hewa ya kaboni dioksidi na kemikali ya methani zinazojitengeneza katika matabaka ya chini ya ziwa.
Vijidudu vinatumia baadhi ya kabondioksidi pamoja na vitu vilivyooza vinavyozama kutoka juu kutengeneza nishati na methani ya ziada.
Gesi hizo kawaida zinatoa maji yanayochemka lakini ziwa Kivu lenye kina kirefu - zaidi ya mita 460 husababisha shinikizo la juu sana kiasi cha kemikali hizo kuyeyuka.
Mchanganyiko huo wa maji na gesi zilizoyeyuka ni nzito kuliko maji ya kiwa peke yake na huyafanya yasipande juu.
Maji ya kwenye kina kirefu cha maziwa pia ni ya chumvi na yenye uchafu unaosababishwa na mvua kutoka tabaka la juu la ziwa na madini ya chemichemi ya maji moto, ambayo yanaongeza uzito wa maji hata zaidi.
Matokeo yake, ni ziwa kuwa na matabaka mengi ya maji yenye uzito mbalimbali na matabaka kidogo tu yenye mianya katikati kulingana na mtaalamu wa maji, Sergei Katsev kutoka chuo kikuu cha Minnesota Duluth.
Lakini ziwa Kivu lina mashaka mengi sana kisayansi, kaboni dioksidi na metahani katika mataba yake ya chini kabisa kumefanya watafiti kuwa na wasiwasi chungu nzima wa uwezekano wa kutokea kwa janga.
Hatari iliyopo
Takriban maili 1,400 kaskazini mashariki mwa ziwa Kivu, ni ziwa lenye bonde la Nyos ambalo pia linakusanya kiwango kikubwa cha gesi iliyoyeyuka - kaboni dioksidi - kutoka kwa bomba la volkeno chini kabisa ya ziwa.
Agosti 21, 1986, kemikali hatari ilijitokeza kwa wingi kutoka kwenye hifadhi ya gesi na kusababisha janga.
Kulitokea maporomoko ya ardhi na ghafla kiwango kikubwa cha maji kikatiririka maeneo jirani na kusababisha kaboni dioksidi kuchanganyikana kwa haraka na matabaka ya juu ya ziwa na kusambaa kwenye hewa.
Kilichotokea ni wingu kubwa la gesi lililosababisha ukosefu wa hewa kwa watu wanaokadiriwa kuwa 1,800 katika vijiji vilivyo karibu.
Wanasayansi wanahofia kwamba tukio kama hilo huenda likatokewa kwa ziwa Kivu na pengine hata baya zaidi.
Wakati mlipuko huyo mbaya unatokea, watu takriban 14,000 walikuwa wanaishi karibu na ziwa Nyos leo hii watu zaidi ya milioni 2 wanaishi maeneo ya karibu na ziwa Kivu.
Wanasayansi wamebaini matabaka ya rangi ya kahawia chini ya ziwa hilo tofauti kabisa na uchafu unaozunguka ziwa. Mtaalamu Katsev anasema uchafu huo usio wa kawaida huenda ukawa sababu ya kulipuka kwa ziwa Kivu.
Aidha, mlipuko unaweza kutokea kwa sababu mbili, ikiwa maji yatachanganyikana kabisa na gesi iliyoyeyuka, yenye kaboni dioksidi au methani ambako kutasababisha mchanganyiko huo wa maji kuanza kuchemka, kupanda juu na kupaa kwenye anga.
Mlipuko pia unaweza kutokea pale shinikizo likisababisha maji ya kina cha chini yenye gesi iliyoyeyuka kutoka na kuchanganyikana na matabaka ya juu, na kupunguza shinikizo la gesi ambapo mchanganyiko hua utatoka mara moja kwa juu na kusambaa kama ilivyo pale
Mtaalamu Katsev anasema mienendo ya ziwa hilo inafuatiliwa sana na iwapo mlipuko utatokea haitakuwa jambo la kusangaza.
Wakati gesi inaendelea kuongezeka katika ziwa la Kivu, hatari zake pia zinazidi kuongezeka. Inasemekana wanasayansi walibaini kwamba kati ya mwaka 1974 na 2004 kiwango cha kaboni dioksidi kiliongezeka kwa asilimia 10.
Lakini wasiwasi mkubwa kwa ziwa Kivu in kiwango cha kemikali ya methani ambacho kiliongezeka kwa asilimi 15 hadi 20 kipindi hicho hicho.
Hata hivyo habari njema ni kwamba gesi hiyo hiyo inayoweza kusababisha janga inaweza kubadilishwa na kuwa chanzo cha nishati katika eneo.
Mwaka 2008, Rwanda ilianzisha mpango wa majaribio wa kuchukua kemikali ya methani kutoka ziwa hilo na kuichoma kama gesi asilia na mwaka jana ilitia saini mkataba wa kuuza kemikali ya methani nje ya nchi.
Mpango wa kubadilisha kwango kikubwa cha kemikali ya methani kwa jina KivuWatt pia ulianzishwa mwaka 2015.
Mradi huo unatoa maji kutoka kwa matabaka ya chini ya ziwa na shinikizo inapopungua kwa maji hayo, gesi inatoka.
Kisha kemikali ya methani inafyonzwa na kutumiwa kama fyueli na kaboni dioksidi inarejeshwa tena kwenye matabaka ya chini ya mto.
"Gesi hiyo inasafirishwa kupitia mabomba na kuichoma kama ilivyoo kwa fyueli za visukuku au mafuta ghafi kuzalisha umeme," Katsev amesema.
Kwa watu wanaoishi karibu, huenda ziwa hilo likawa chanzo kizuri cha nishati.
Mpango wa KivuWatt ukikamilika, megawati 100 za nishati zitazalishwa katika mpango huo kutabadilisha maisha ya raia wa Rwanda nchi ambayo asilimia 35 pekee ya idadi ya watu wake ndio wenye kupata umeme.
Kubadilisha gesi za ziwa Kivu huenda kukasaidia kupunguza hatari za kulipuka kwa ziwa hilo ingawa hilo haliwezi kuondolewa kabisa.