Second lady kunako lebo ya muziki ya Wasafi Classic baby (Wcb), zuhura othman Soud ‘Zuchu’, anadaiwa kumtia adabu msanii mwenzake wa Bongo Fleva na mwanamitindo, Hamisa Mobeto ‘Misa’. Zuchu anadaiwa kumzidi kete Mobeto kwenye ngoma zao walizoachia kwa kuviziana wikiendi iliyopita.
ISHU IKO HIVI…
Zuchu na Mobeto wameongozana kuachia ngoma zao kwa mpigo, ambazo zote ni kolabo za kimataifa, lakini Zuchu amefanikiwa kumfunika Mobeto na kumshikisha adabu, kwa kumzidi mwendo.
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limekwenda hatua kwa hatua, katika kutazama ni nani mwenye ubavu wa kumkimbiza mwenzake.Oktoba 14, mwaka huu, Mobeto aliachia wimbo wake mkali unaokwenda kwa jina la Ginger Me, akiwa amemshirikisha staa wa muziki kutoka nchini Nigeria, Singah.
Wimbo huo umekimbiza na unaendelea kukimbiza kwenye Mtandao wa YouTube na mitandao mingine ya kusikiliza, kutazama na kuuza muziki kwa muda mchache kabla ya kushushwa na Nobody wa Zuchu.
Zuchu ambaye ana muda mfupi kwenye gemu, lakini amefanya mambo mengi makubwa ikiwemo kutajwa kuwania tuzo kubwa duniani za Grammy, Oktoba 16, mwaka huu aliachia wimbo wake wa Nobody akiwa na mwanamuziki mkubwa kwa sasa nchini Nigeria, Joeboy.
ZUCHU AMKIMBIZA MOBETO
Wimbo huo wa Zuchu ulikimbizana na wa Mobeto kwa saa chache kabla ya Zuchu kusimama kileleni kwa kushika nafasi ya juu au ya kwanza (trending) na kukaa namba moja kwa kutazamwa zaidi ya mara laki saba kwenye Mtandao wa YouTube, huku wa Mobeto ukitazamwa zaidi ya mara laki mbili tu!
Mpishano huo mkubwa wa data, ulimfanya Zuchu aonekane kupiga hatua na kumzidi mwendo Mobeto kwa kuendelea kukimbiza hata kwenye mitandao mingine ya kuuza, kupakua na kusikiliza muziki (platforms) mbalimbali duniani.
KOLABO ZA KIMATAIFA
Joeboy aliyeshirikishwa na Zuchu, ni msanii ambaye yuko moto kwa sasa Afrika na duniani kote, kutokana na kipaji chake kikali.Kitendo cha kukutana na Zuchu, imekuwa ni bonge moja la kemstri na ndiyo sababu wimbo wao umeendelea kukimbiza na kuwa gumzo kwa muda mfupi.
wa upande wake, Singah aliyeshirikishwa na Mobeto, ni msanii mkali pia na yuko chini ya rekodi lebo ya mwanamuziki mkubwa nchini Nigeria aliyekuwa akiunda Kundi la P-Square, Peter Okoye ‘Mr P’.
MASHABIKI WANASEMAJE
Baadhi ya mashabiki mitandaoni walichangia maoni yao kuhusiana na kolabo hizo, ambapo wamesema Zuchu siku zote haotei bali anatoa kazi kali, hivyo Mobeto akasome!
“Tangu Zuchu aingie kwenye muziki amekuwa akiwanyoosha kweli, ona sasa ametoa ngoma kali na msanii mkubwa kama Joeboy na inakimbiza mno mitandaoni, Hamisa anatakiwa achukue somo hapa,’’ anasema mmoja wa mashabiki wao akimtaka Mobeto kukaza buti.
“Zuchu amejua kumtia adabu Hamisa (Mobeto) maana yeye alianza, mwenzake akaja kufunga mjadala kabisa na ngoma kali,’’ aliandika shabiki mwingine kwenye ukurasa wa Zuchu.
Zuchu bado anaendelea kubaki kileleni kwa kukimbiza na ngoma zake nyingine za Cheche na Litawachoma akiwa na bosi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’.“Kwa makala ya uchambuzi wa kina kuhusiana na nyimbo zao, funua ukurasa wa 8&9)
Stori: Happyness Masunga