Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera ameponda mbinu za kujihami za kocha Cedric Kaze ambazo anadai ndizo zilizosababisha wanajangwani kutopata ushindi dhidi ya wekundu wa msimbazi Simba katika dabi ya Kariakoo iliyochezwa siku ya jumamosi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Zahera ambaye kwasasa ni Mkurugenzi wa ufundi wa Gwambina FC amesema kwa ubora wa wachezaji walionao Yanga hawakupaswa kujihami dhidi ya Simba ambayo tayari ilionekana kuutawala mchezo katika kipindi cha pili.
''Mimi nilishangaa sana, Yanga ilikuwa inaongoza na walikuwa wanacheza vizuri ajabu Kaze akaamua kubadili mbinu na kuiruhusu Simba kuuchukua mchezo, kwakweli hawakupaswa kurudi nyuma''.
Kwa upande wa Simba, Zahera amesema kwamba ilicheza vizuri kwa kupiga pasi fupi fupi lakini wanatatizo katika idara ya kiungo haswa kwa Clatous Chama na Jonas Mkude ni wachezaji wanaocheza taratibu sana.
''Simba inacheza vizuri kuanzia katika eneo la ulinzi, na wanawashambuliaji wenye kasi kama Benard Morrison na Luis Miquissone, hawa wanahitaji mpira kwa haraka, lakini Chama na Mkude wapo taratibu sana, na hii itawagharimu katika michuano ya kimataifa'' alisema Zahera.
Yanga ilitangulia kupata bao dakika ya 31 lililofungwa na Michael Sarpong kwa penati kufuatia mlinzi wa Simba, Joash Onyango kumuangusha Tuisila Kisinda katika eneo la hatari, lakini Onyango alisawazisha dakika ya 86 kwa kichwa akiunganisha kona ya Luis Miquissone.