Waendesha mashitaka nchini Argentina wanamchunguza daktari wa Diego Maradona kwa uwezekano wa kuua kufuatia kifo cha nyota huyo wa soka kilichotokea siku nne zilizopita.
Polisi wapatao 30 walivamia makazi ya daktari Luque Jumapili asubuhi, huku wengine 20 wakienda katika kliniki yake iliyopo katika mji mkuu Buenos Aires wakijaribu kubaini iwapo ulikuwepo uzembe katika matibabu baada ya upasuaji aliofanyiwa Maradona.
Maradona ambaye alikuwa na umri wa miaka 60 alifariki dunia kutokana na shambulio la moyo nyumbani kwake ambako alikuwa akiendelea kupona baada ya kufanyiwa upasuaji.
Polisi pamoja na waendesha mashtaka wanashuku kwamba nyota huyo wa soka kuruhusiwa kwake kwenda nyumbani hakukutimiza vigezo vya kumruhusu atoke hospitalini, ikiwemo kupewa wauguzi au nesi wa kumuhudumia saa 24.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliogubikwa na hisia Jumapili, Dkt Luque ambaye alielezewa kama daktari wa kibinafsi wa Maredona, aliangua kilio akisema kuwa alifanya kile alichoweza kuyanusuru maisha yake ya rafiki yake. Alisema kuwa Maradona alikuwa ni mwenye huzuni katika siku za hivi karibuni.