Azam vs Yanga… Vita ya Rekodi Bongo




LEO Jumatano kwenye Uwanja wa Azam Complex, Azam FC itakuwa na kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Yanga huku vita kubwa ikiwa ni kwa wachezaji kusaka rekodi mpya ndani ya uwanja.

 

Kwa upande wa ushambuliaji, balaa litakuwa kwa Prince Dube mwenye mabao sita na pasi nne za mabao kati ya 18 yaliyofungwa na Azam FC, atakuwa akipambana na Michael Sarpong wa Yanga mwenye mabao matatu kati ya 13 kwenye kuongeza idadi ya mabao ya kufunga na kuwania kiatu cha ufungaji bora.

 

Upande wa vita ya walinda mlango, David Kisu wa Azam FC, vita yake ni kwenye kusaka clean sheet (mechi bila kuruhusu bao) ambapo akiwa amekaa langoni mechi 11 amekusanya clean sheets saba na kufungwa mabao matano kwenye mechi nne na Metacha Mnata yeye amekaa langoni mechi 10 na kukusanya clean sheets saba na kufungwa mechi tatu katika kikosi cha Yanga.

 

Kwenye ulinzi, Bakari Mwamnyeto, safu yake ya ulinzi ya Yanga imeruhusu mabao manne yakiwa ni machache kuliko yale ya Azam FC inayoongozwa na Yakubu Mohamed iliyoruhusu mabao matano kwenye mechi 11.

 

Nyota hawa wawili watakuwa na kazi ya kulinda rekodi zao na kuweka rekodi mpya kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa Mwamnyeto kuvaa jezi ya njano akipambana na Yakubu kwa kuwa awali alikuwa Coastal Union ya Tanga.

 

Viungo, kwa Azam FC ni mzawa Mudhathir Yahya mwenye pasi moja ya bao, atapambana na Carlos Carlinhos raia wa Angola mwenye mabao mawili na pasi mbili za mabao katika kikosi cha Yanga.

 

Kuelekea mchezo huo, Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’, amesema: “Katika mchezo wetu wa Jumatano, mwalimu amekiandaa vyema kikosi chake kuwakabili Yanga, tunajua ni timu nzuri ina wachezaji wazuri na hata sisi kwa upande wetu tumejiandaa kuhakikisha tunaendelea kubaki kileleni ili mwisho wa siku tutimize lengo.

 

“Tumejiandaa vizuri na mwalimu atawatumia wachezaji wetu wote ambao hawakucheza mechi yetu dhidi ya KMC akiwemo Nicolas Wadada na Ally Niyonzima ambao walikuwa wakizitumikia timu zao za taifa, pia Sure Boy yeye aliumia, lakini sasa yupo vizuri, atacheza dhidi ya Yanga.”

 

Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Cedric Kaze, amesema kuanzia mchezo huo wa leo, amekuja na mpango mpya wa kusaka mabao.

 

“Kwa sasa tunatakiwa kutafuta njia za kufunga mabao zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo tuna mwendo wa kufunga kwa idadi ndogo.

 

“Tunataka kufanya hivyo kwa sababu ya kumaliza vizuri katika mechi zetu hizi zilizobaki kabla ya ligi kumaliza mzunguko wake wa kwanza,” aliweka nukta Kaze.

GPL
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad