Azam vs Yanga… Vita ya Wakubwa, Kaeni Mbali




JIJI la Dar es Salaam, kwa mara nyingine leo Jumatano litakuwa kimya kwa muda kupisha mechi ya wakubwa wawili, Azam na Yanga ambao watakuwa kwenye Uwanja wa Azam Complex wakisaka pointi. Mechi hii inazikutanisha timu hizi ambazo zinawania kukaa kileleni mwa ligi kuu.

 

Ndani ya dakika 90 za mechi hii, kuna mambo mengi ambayo yanatarajiwa kutokea kama makala haya yanavyokuchambulia baadhi ya vitu ambavyo vitanogesha.

 

UFALME WA KILELENI

Mwisho wa dakika 90 za mechi hii zitaamua nani ataenda kileleni na mwingine atakaa kwenye nafasi ya pili. Msimamo wa ligi unaonesha kwamba timu hizi zote zina pointi 25, lakini Azam ipo kileleni ikiwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo mshindi wa mechi hii atakusanya pointi na kwenda mbali kumzidi mwenzake.

 

Kipengele hiki kinazidisha ugumu wa mechi hii na kuifanya kuwa na mvuto wa kipekee kwa mashabiki wengi kutamani kujitokeza uwanjani kwenda kuangalia nani atakwea kileleni na kumuacha mpinzani wake nafasi ya pili.

 

KISASI CHA YANGA

Mechi hii ni ya kisasi kwa Yanga kwa sababu msimu uliopita waliambulia pointi moja pekee kwenye pointi sita ambazo walipambania mbele ya Azam.

 

Kwenye mechi ya kwanza Yanga walipoteza kwa kufungwa bao 1-0, mlinzi Ally Mtoni ‘Sonso’ akijifunga huku katika mechi ya pili ikimalizika kwa suluhu.

 

Kwa hiyo msimu huu Yanga watakuja kwenye mechi hii wakiwa na hasira zaidi za kutaka kushinda na kufuta rekodi mbovu ya kutowafunga wapinzani wao kwani kwenye mechi tatu za mwisho, hawajashinda hata moja. Mbili za msimu wa 2018/19 na moja ya msimu wa 2017/18.

 

FURAHA YA SIMBA

Mechi hii kwa kiasi kikubwa ni furaha ya Simba kwa sababu matokeo ya namna yoyote ile kwao yatakuwa wanayafurahia. Kama mechi ikiisha kwa sare, wote watakuwa na pointi 26, huku Simba wakiwa na pointi 23 na mechi moja mkononi.

 

VITA YA KIMBINU, MIFUMO

Pambano hili litakuwa la kiufundi zaidi kwa makocha wa timu zote mbili. Makocha wote wawili ni waumini wa soka la chini na wamekuwa wakifanya hivi hasa wanapocheza kwenye uwanja wenye ubora.

 

Kitu kingine ni mifumo inayotumiwa na vikosi hivi kuonekana kufanana na kubadilika kutokana na mpinzani anavyokuwa. Kaze mara nyingi anatumia 4-3-3 kisha 4-4-2 kama ambavyo Cioaba anavyopenda kutumia mifumo hiyo.

 

MASTAA WAPYA MTEGONI

Mastaa wapya waliosajiliwa na klabu hizi mwanzoni mwa msimu, hii ni mechi yao ya kuonesha uwezo wao. Azam waliwasajili Prince Dube, Akono Akono, Awesu Awesu, David Kissu, Ismail Kader, Ally Niyonzima ambao kwenye mechi hii wanatakiwa kuonesha thamani yao wakati Yanga wakiwa na Farid Mussa, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Yassin Mustapha, Kibwana Shomary, Carlos Carlinhos, Yacouba Songne na Michael Sarpong.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad