Mwenyekiti wa Tume ya Maridhiano Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum, amewasihi Watanzania kuendelea kumshukuru Mungu baada ya uchaguzi mkuu kufanyika salama na kwa amani na kilichobaki ni kuendelea kuiombea Serikali iliyoshinda iongoze vyema.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma na kusema kuwa inatakiwa sasa baada ya uchaguzi kumalizika salama ni kuungana na kuendelea kuiombea kwa Mungu serikali iliyoshinda iongoze vyema.
"Katika chaguzi zote kuna kushinda na kushindwa, huwezi kukubalika na kila mmoja haiwezekani, manabii wa Mwenyezi Mungu na hata wacha Mungu hawakukubalika nao walipingwa hii ni desturi ni jambo la kawaida", amesema Sheikh Alhad.
Aidha Sheikh Alhad akatoa ushauri, "Kubwa tunawaomba Watanzania nchi yetu iendelee kuwa salama na utulivu, tunahitaji nchi yenye amani ili tuweze kufanya shughuli zetu kwa ukamilifu bila bughudha yoyote, tusijaribu kuchezea amani iliyopo, tutajuta, tuna mifano mingi ya nchi mbalimbali zilizochezea amani, kuirejesha ni ngumu sana".