MCHEZAJI wa Simba, Bernard Morisson kwa utundu kashindikana aisee! Unajua kwa nini, safari hii kaangukia kwa mrembo Amber Lulu.
Imekuwaje? Jamaa ambaye ni raia wa Ghana kaonekana juzi kati kwenye klipu ya video iliyosambaa mitandaoni akifaidi na mwanamke huyo wa mjini kwenye viunga vya klabu moja jijini Dar es Salaam.
Tukio hili linakuja miezi mitatu tangu picha tata za Morrison na msanii Linah Sanga kusambaa mitandaoni na kuzua utamu wa mahaba ambayo baadaye wahusika waliyakana.
Linah ambaye majina yake kamili ni Esterlinah Sanga baada ya kusambaa kwa picha hizo akiwa na Morrison aliulizwa “katoa tuzo kwa mchezaji huyo” ambapo alisema
“Nilikuwa kwa mmoja wa marafiki zangu maeneo ya Kawe (jijini Dar) ndipo Marrison nilijikuta, nikiwa kama shabiki damu wa Simba na shabiki wa mchezaji huyo niliona tupige picha ya kumbukumbu.”
Baada ya ufafanuzi huo wa Linah ni kama mjadala ulifungwa kiaina na kuwaacha watu wakiendelea ‘ku-zuum’ picha za wawili hao.
Kama Waswahili wasemavyo; jasiri haachi asiri yake, mtundu Morrison juzikati kakichafua tena kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuonekana akiwa na Amber Lulu huku mshikaji akimfanyia mwanamke huyo ‘uchokozi’.
Mmoja kati ya watu waliokuwepo kwenye ukumbi huo usiku wakati mchezaji huyo akijiachia na mwanamke huyo aliliambia RISASI MTANDAONI kuwa; “Ulikuwa usiku wa wawili hao kujivinjari laivu.”
Hata hivyo, tofauti na Linah ambaye alisema kuwa ni shabiki wa Morrison, Amber Lulu hayuko kwenye taipu hiyo kwani alionekana kutomfahamu vizuri mchezaji huyo wa Simba kwa madai kuwa yeye siyo mtu wa mpira hiyo ni kwa mujibu wa chanzo chetu.
Wanaojiongeza kwa kuunganisha vidoti vya matukio walifika mbali na kusema kilichokuwa kikiendelea kwa mchezaji na msanii huyo ni mahaba na si vinginevyo.
Amber Lulu alipotafutwa kwa njia ya simu na mwandishi wetu kuulizwa siku ya tukio “aliamkia wapi?” Hakupatikana.
Hata hivyo, Morrison ambaye naye hakupatikana alipotafutwa, hakuwashtua mashabiki wa Simba kwa tukio hilo kutokana na kutokuwepo kwenye kikosi kitakachocheza na Yanga, Novemba 7, mwaka huu, tofauti na hapo yangemkuta mazito.
Mchezaji huyo anatajwa kuwa ni mtu anayependa kujichanganya na watu mbalimbali bila kujali madaraja yao na kwamba amekuwa akiwafurahisha mashabiki zake ambao wamempa jina la “mzee wa kuwakera.”
Kama na tukio hili la kumfanyia utundu Amber Lulu, usiku litawakera watu basi mchezaji huyo atakuwa analitumikia vyema jina lake jipya.
STORI: MWANDISHI WETU