USICHEZE na serikali weweee! Siku chache baada ya bilionea wa ajabu aitwaye Agustino Njaku kutikisa mkoa wa Ruvuma na serikali ya mkoa kumtia mtu kati kwa uchunguzi; taarifa mbichi ni kwamba akaunti za benki za bilionea huyo zimekatwa.
Taarifa za kukamatwa kwa akaunti za Njaku na washirika wake wanaomiliki kampuni ya Njaku Ltd, zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye; huku sababu ya kufanya hivyo ikitajwa kuwa ni kufanya uchunguzi.
“Ni kweli tumezifunga akaunti hizo ili tuchunguze kiasia ambacho kipo kwenye akaunti kama kinatosheleza kuwalipa wananchi wanadai.
“Kama tukijilidhisha tutajiachia na watu wataendelea kulipwa haki zao, kikubwa wanaodai fedha zao wavumilie kwa muda wakati tunakamilisha uchunguzi wetu,” alisema mkuu huyo wa wilaya alipozungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kuzuiwa kwa akaunti za bilionea huyo aliyejitwalia umaarufu hivi karibuni kwa kile ninachotajwa kuwa ni uwezo wa kununua mahindi ya wakulima kwa bei kubwa na kuyauza kwa bei ndogo, jambo ambalo limekuwa likiwashangaza wengi.
Mbali na ununuzi huo wa mazao kwa staili ya ajabu, Njaku na wenzake watatu waliojitwalia heshima ya ubilionea wamekuwa wakigawa fedha kwa wananchi kama njugu kwa kile wanachodai kuwa ni “kuwawezesha kimaisha.
Kufuatia sarakasi za mabilionea hao, hivi karibuni kulizuka malalamiko kuwa kuna baadhi ya watu wanachukuliwa mazao yao bila kulipwa jambo lililowafanya polisi kumtia mbaroni Njaku ambaye ndiyo kinara wa kundi hilo la watu wanaojiita matajiri wa mazao.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni kamanda wa Polisi Mkoa huo… alisema uchunguzi wa madai hayo uko ngazi ya wilaya na kwamba unafuatiliwa na vyombo vyote vya usalama ikiwemo Takukuru, Usalama wa Taifa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
“Kimsingi yule mtu alikuwa ananunua mazao na kuuza wakati huo Mamlaka ya Mapato ‘TRA’ pamoja na manispaa walikuwa wanachukua ushuru, sasa huwezi kusema watu hao ni matapeli.
“Lakini kwa sababu idara za usalama zinafuatilia, nisiwe msemaji, kuna kamati ameundwa na mkuu wa mkoa ambaye ni bosi wangu,” alisema kamanda huyo
Huwenda kutokana na uchunguzi huo ndiyo uliofanya akaunti za bilionea Njaku kufungwa kwa muda ili kujilidhisha kama anao uwezo wa kutosha kuwalipa watu wote waliomuuzia mazao yao hasa mahindi na maharagwe au la!
Awali ilielezwa kuwa, Njaku akiwa kama bosi wa kampuni ya Njaku Ltd na wenzake wamekuwa wakinunua mazao kwa wakulima kwa bei kubwa na kuwauzia wananchi kwa bei nafuu.
Kwa mujibu wa mamlaka za serikali ni kwamba Njaku na wenzake wanaofahamika kama “wafanyabiashara wa mazao” walioomba kibali cha kununua mazao ya wananchi kama mahindi na maharagwe ambacho wamepewa kihalali. Hata hivyo, kinachokuna vichwa vya wengi ni namna wafanyabiashara hao wanavyonunua mazao kwa bei ya juu na kuyauza kwa bei nafuu.
Imeelezwa kuwa, Njaku na wenzake walianza ununuzi wa mazao kama mzaha ambapo waliweza kununua gunia la mahindi kwa bei shilingi elfu sitini (60,000) na kuliuza kwa wafanyabiashara mbalimbali kwa bei ya shilingi elfu arobaini na tano (45,000).
Baadaye waliongeza dau kwa kununua gunia la mahindi lenye kilo 120 kwa bei ya shilingi elfu sabini na tano (75,000) na kuliuza kwa bei ya shilingi elfu arobaini na tano (45,000). Ununuzi na uuzaji huu wa nafaka umekuwa ukiwaacha wengi midomo wazi na hasa namna wafanyabiashara hao wanavyoweza kupata faida.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwepo kwa shehena kubwa ya mazao kwenye ghara linalomilikiwa na mabilionea hao ambayo wahusika wanadai hawajalipiwa fedha zao