MWANASIASA maarufu wa upinzani nchini Uganda ambaye pia ni msanii wa muziki, Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’, ameteuliwa rasmi kugombea urais nchini humo katika uchaguzi mkuu wa mwakani 2021.
Wine aliwasili kwenye kituo cha uteuzi akiwa ameandamana na mke wake, baada ya hati zake kukaguliwa, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Justice Simon Byabakama alisema, “Tumethibitisha hati zilizowasilishwa na mgombea kwamba ametimiza vigezo vyote vya uteuzi.”
Sasa ni rasmi kuwa Wine atakabiliana na Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu mwaka ujao mwaka 2021. Wine pia alikumbushwa kwamba mikusanyiko ya umma bado imepigwa marufuku na kwamba kampeni zake zote zitaendeshwa kulingana na miongozo ya tume ya uchaguzi.
Wakati huohuo, Ubalozi wa Marekani Kampala umetoa tahadhari ya usalama kwa raia wake mjini Kampala ambapo umeshauri raia wake kujizuia kufika maeneo ya mji wa Kampala na karibu na eneo la Kyambogo kwa sababu ya uwezekano wa kutokea kwa ghasia Jumanne kunakohusishwa na shughuli ya uteuzi wa urais.
Kabla ya kutoka nyumbani kwake, Bobi Wine alisema kuwa atazungumza na vyombo vya habari na amekubali kwenda na watu kumi kama inavyotakiwa na Tume ya Uchaguzi ya Uganda. Hata hivyo, inasemekana kwamba jeshi la polisi limezunguka ofisi za chama cha Bobi Wine cha National Unity Platform (NUP).
Pia hali ya usalama imeimarishwa katika mji wa Kampala na vitongoji vyake. Jana Museveni alikuwa miongoni mwa walioteuliwa na kupata fursa nyengine ya kutetea kiti chake kwa muhula mwingine.
Muda mfupi baada ya kuteuliwa na kutangazwa kuwania urais, jeshi la Polisi nchini Uganda limemkatama Bobi Wine na msemaji wake, Joel Ssenyonyi, na kupelekwa kusikojulikana.