Mkutano wa kwanza wa Bunge la 12 umeanza leo jijini Dodsoma wakati Watanzania wakiwa na shauku ya kufahamu nani atateuliwa kuwa waziri mkuu wa Tanzania katika muhula wa pili wa uongozi wa Dk John Magufuli.
Kwa mujibu wa katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai miongoni mwa shughuli zitakazofanywa katika Bunge hilo leo ni kusomwa kwa tangazo la Rais kuliitisha Bunge hilo kwa ajili ya kujadili maendeleo ya wananchi, kutunga sheria mpya pamoja na kuzibadili zilizopo.
Kagaigai alisema baada ya kusomwa kwa tangazo la Rais, utafanyika uchaguzi wa spika na naibu wake, nafasi zinazotetewa na waliokuwapo, Job Ngugai kutoka Jimbo la Kongwa na Dk Tulia Ackson aliyechaguliwa kuwakilisha Mbeya Mjini.
Baada ya uchaguzi huo na spika kula kiapo, wabunge wateule nao, wawakilishi 264 waliochaguliwa majimboni pamoja na 105 wa viti maalumu watano kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wataapa.
Shughuli nyingine kubwa itakayofanyika leo ni kuthibitisha jina la waziri mkuu litakalowasilishwa bungeni na Rais John Magufuli.
Ingawa Rais Magufuli amewahakikishia wateule wa Serikali aliohudumu nao katika miaka mitano ya kwanza kuendelea na nafasi za uteuzi walizokuwa nazo, bado Watanzania wanasubiri kujua kama atafanya mabadiliko yoyote katika nafasi muhimu ya waziri mkuu ama la.