IMEFAHAMIKA kuwa kiungo mchezeshaji raia wa Zambia, Clatous Chama, amekataa mkataba wa miaka miwili Simba wenye dau la Sh milioni 150 huku watani wao wa jadi wakimtengea Sh milioni 300.
Kiungo huyo fundi, hivi karibuni ilielezwa amegomea mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuichezea Simba huku akiwataka viongozi kusubiria hadi mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu. Yanga hivi karibuni ilielezwa imeanza mazungumzo ya siri na meneja wa kiungo huyo kwa ajili ya kuhitaji huduma yake msimu ujao baada ya mkataba wake kumalizika Simba.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatau, Yanga imerejea kimyakimya kwa meneja wa kiungo huyo kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya awali ili wafanikishe mipango yao ya kumsajili Chama ambaye ni tegemeo hivi sasa kwenye kikosi cha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck.
Mtoa taarifa wetu alisema kuwa kiungo huyo wiki iliyopita kabla ya mchezo wa Dar es Salaam Dabi, alifanya kikao na Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya mwisho ya kukamilisha dili hilo la usajili.
Aliongeza kuwa mabosi wa Simba wamemuwekea kitita cha Sh 150Mil ambacho alitengewa ili asaini na kugoma huku akiomba kuongeza mkataba huo mwishoni mwa msimu.
“Vita kubwa ipo ya kimyakimya kati ya vigogo wa Simba na Yanga ambao wote wanawania saini ya Chama katika msimu ujao, licha ya kuwepo taarifa za kukanusha kuwa nyota huyo anaendelea kubakia Msimbazi.
“Siku moja kabla ya mchezo Dar es Salaam Dabi viongozi wa Simba walifanya kikao na Chama, katika kikao hicho viongozi hao wameonekana kumshawishi kiungo huyo asaini mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh milioni 150.
“Wakati Simba wakitaja dau hilo, Yanga wenyewe wanafanya mipango yao kimyakimya ambao wenyewe wapo tayari kumpa Sh milioni 300 ili asaini mkataba wa miaka miwili Jangwani,” alisema mtoa taarifa huyo.
Chama alilaumiwa na mashabiki wengi wa Simba kwa kucheza chini ya kiwango katika pambano dhidi ya Yanga Jumamosi iliyopita. Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Mashindano wa Yanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said hivi karibuni alisikika akisema: “Kama uongozi tupo tayari kusajili mchezaji yeyote atakayependekezwa na kocha.
“Kikubwa hatutaki kumuingilia kocha wetu katika masuala yote yanayohusiana na usajili, hakuna mchezaji tutakayeshindwa kumsajili katika kuelekea usajili wa dirisha dogo.”