Chama Awekewa Ulinzi Mkali Zambia

 

SIMBA wameanza kupata hofu na kiungo wao Clatous Chama baada ya kumwekea ulinzi kila mahali ili asinaswe na wapinzani wao.


Kumekuwa na taarifa mbalimbali kuhusu kiungo huyo mahiri zaidi hapa nchini kwa sasa, lakini suala la kutosaini mkataba mpya kwenye timu hiyo limezua gumzo zaidi.


 


Mkataba wa Chama na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu huu na kuna taarifa kuwa wapinzani wao wakubwa hapa nchini, Klabu ya Yanga inamtaka mchezaji huyo raia wa Zambia asaini kwao atakapomaliza mkataba.


 


Chama kwa sasa yupo nchini kwao Zambia alipokwenda kuitumikia timu yake ya Taifa ambayo itacheza mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2020) dhidi ya Botswana leo Alhamisi na watarudiana wikiendi ijayo.


 


Chanzo kimelieleza Spoti Xtra kuwa, Simba wamemwekea ulinzi mkali kiungo huyo akiwa na timu ya taifa na hatatakiwa kuzungumza na mtu yeyote zaidi ya wale wa timu ya Zambia.


 


Inaelezwa kuwa, Simba wamepata hofu kuwa wapinzani wao wanaweza kukwea ndege kwenda Zambia au kuwatumia watu wa pale kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mchezaji huyo kwa kuwa hapa jijini Dar es Salaam imekuwa ngumu kufanya hivyo.


 


Simba wamedaiwa kuwa wamefanya mazungumzo na marafiki zao kadhaa ambao wapo Zambia wakiwataka kufuatilia kila kitu kuhusu mchezaji huyo na kuzuia njama zozote ambazo zinaweza kutokea.


 


“Mambo ni magumu, Simba wamepata hofu sana lakini wameweka pia ulinzi mkali kuhusu mtu yeyote ambaye anaweza kuzungumza na Chama kwa kuwa wanaamini huku inaweza kuwa rahisi.


 


“Wamezungumza na baadhi ya watu wao huku Zambia na kuwataka kumlinda kiungo huyo asije akazungumza na mtu yeyote ambaye yupo nje ya kambi ya timu hiyo.


 


“Hata hivyo, bado wana hofu kwa kuwa kuna baadhi pia ya watu ambao wapo hapa Zambia ambao wapo karibu sana na wapinzani wao na wanahofia kuwa wanaweza kufanya mbinu yoyote.


 


“Lakini pia kuna chanzo kinasema kuna kiongozi anaweza kuja hapa kutoka huko Tanzania kwa ajili ya Chama, sasa sijajua ngoja nifuatilie,” kilisema chanzo hicho bila kutaja ni kiongozi wa timu gani.


 


Mbali na Yanga, pia inaelezwa kuwa Chama anawindwa na timu kadhaa kubwa zikiwemo za Afrika Kusini, Misri na DR Congo, hivyo Simba hawataki mtu yeyote aongee na kiungo huyo ambaye ameshafunga mabao mawili na kutoa pasi tano za mabao katika Ligi Kuu Bara msimu huu.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad