ELIZA EdwidarrBy Elizabeth Edward
Dar es Salaam. Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam unajipanga kuanza upya kazi ya kuwaondoa ombaomba baada ya kumalizika kwa mchakato wa uchaguzi mkuu.
Akizungumza na Mwananchi jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Jumanne Shauri alisema pamoja na kutingwa na jukumu la uchaguzi mkuu, mlipuko wa ugonjwa wa virusi vyacorona uliwafanya wasitishe kazi ya kuwakusanya ombaomba hao kutoka katikati ya jiji.
“Tulianza vizuri lakini tulikazimika kusitisha kwa sababu ya corona. Ilikuwa ni hatari kuwajaza kwenye gari moja tukaona tuache kwanza na wao wakaona ndio fursa ya kujiachia mjini.
“Hilo limeisha, ukaja uchaguzi sasa zile pilikapilika za maandalizi hadi uchaguzi wenyewe kufanyika na kumalizika hatukuwa na muda wa kufuatilia. Sasa tumerudi kazini muda wowote tunakwenda kusafisha mji,” alisema Shauri.
Shauri alisema kazi hiyo itaendeshwa kwa kushirikiana na Polisi ambao watakuwa macho kwenye makutano ya barabara za jiji kuangalia kuwanasa ombaomba na wanaowapatia fedha au vitu.
Kuhusu wanaotaka kusaidia watu hao, Shauri alieleza misaada hiyo ielekezwe kanisani, misikiti au kwenye makazi ya watoto yaliyopo Msongola na Vingunguti.
Mapema mwaka huu, Manispaa ya Ilala ilitambulisha sheria ndogo ya kukabiliana na ombamba ambayo inawabana pia wanaowasaidia watu hao. Licha ya mara kadhaa ombaomba hao kuondolewa, baada ya muda wamekuwa wakirejea.