Na Thabit Madai,Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi leo Novemba 21, 2020 amewaapisha mawaziri 13 wa baraza la mawaziri la serikali ya awamu ya nane na kuwaapa magizo 13 ya kuanza nayo kazi katika Wizara zao.
Hafla hiyo ya uapisho wa mawaziri hao imefanyika katika viwanja vya Ikulu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na viongozi wa madhehebu mbalimbali Dini.
Dk. Mwinyi aliwambia mawaziri hao kuwa wahakikishe kila mmoja anaijua Wizara yake na Taasisi zilizo chini ya Wizara husika haraka iwezekanavyo kwa kuzitembelea na kutatua changamoto zilizopo.
"Ukweli kuwa katika wizara na Idara munazokwenda kuzisimamia kuna changamoto nyingi, hivyo kila mmoja wenu ahakikishe kuwa anakwenda sasa anakwenda kuzitembelea idara na taasisi zilizopo chini ya wizara husika na kutatua changamoto," alisema Rais Dk.Mwinyi.
Pia Rais, Dk.Mwinyi aliwambia mawaziri hao kuwa watengeneze Mpango kazi na Bajeti kwa kutumia ilani, hotuba ya Raisi, ahadi zake wakati wa kampeni, Wapate maoni ya Wadau wa wizara pamoja na kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020/2050.
"Mara baada ya hafla hii ya kula kwenu kiapo, mutapewa kitabu kutoka ofisi yangu chenye ahadi yangu wakati wa kampeni ili mutumie wakati wa kutengeneza mpango kazi na bajeti," alisema Dk. Hussein Mwinyi.
Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kila Waziri ahakikishe anatembelea miradi yote inayotekelezwa na wizara husika kwa kuangalia ubora, utaratibu wa zabuni, malipo yaliyofanyika na muda wa kumalizika kwa miradi.
“Katika hili nataka nitoe mifano kidogo, kwa kipindi kifupi nilichokaa katika kiti hichi,nimetembelea baadhi ya maeneo na kukuta miradi inayotekelezwa ipo kiwango ambapo nimesikitishwa sana na kiwango cha miradi tunayoifanya, mkandarasi ameshalipwa fedha zote, nataka maelezo ya kina juu ya mradi ule” Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi – Rais wa Zanzibar
Hata hivyo Dk. Mwinyi alisema kuwa mawaziri hao wahakikishe kwamba anasiamamia uwajibikaji kwa watendaji wa taasisi za umma ambapo kila mmoja awajibike kwa kazi aliyopewa pamoja na kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa kama inayotakiwa.
Alisema kuwa mawaziri wanawajibu wa kuhakikisha haki za watu zinatolewa ikiwa kwa wafanyakazi walipwe posho zao, fedha za Safari zitolewe pamoja na pesa za muda wa ziada wa kazi (overtime).
"Mfano Mzuri katika Wizara ardhi kuna matatizo mengi, wekeni muda wa kuwasikiliza watu matatizo yao na kuwatatulia, ninayo taarifa kwamba katika kipindi cha kampeni kuna maeneo ambayo yalipimwa na kutolewa hivyo nahitaji taarifa ya kina,"alisema Dk.Mwinyi.
Rais Dk. Mwinyi aliwaambia kwamba, wahakikishe kunapatikana kwa Utawala bora na kuondoa Rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma huku wakipambana na wiza utokanao na makusdanyo za bajeti na fedha za miradi zinazotumika vibaya.
"Waziri akishindwa kuayashughulikia haya maana yake hanifai, nataka niwaambie kwamba ukifanya vizuri utabaki na ukifanya vibaya utaondoka, tuliwaahidi wananchi lazima tutekeleza, " alisisitiza Dk.Mwinyi.
Hata hivyo aliwasisitiza kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya Serikali huku akiwaambia kuwa Wizara ya fedha kuwa karibu na vyombo vinavyohusika na makusanyo ya Fedha ZRB na TRA viangaliwe.
"Wizara ya Ardhi kuna makusanyo yatokanayo na kodi za viwanja, na makusanyo mengi pake fedha zinapotea, Wizara ya maliasiri wale wanaopewa vibali vya mchanga kuna pesa nyingi zinapotea, rekebisheni hayo mara moja,"alisema Dk. Mwinyi.
Aliendelea kuwaambia mawaziri hao kuwa wabunifu katika utendaji wao wa kazi ambapo aliwaambia kila mmoja abuni mambo mapya katika utendaji wake wa kazi kwa kuwatumia wataalamu waliopo katika wizara zao.
Rais,Dk. Mwinyi aliongeza kwa kuwataka kuondoa urasimu kwa kuwaondolea usumbufu wananchi wakati wa kupata huduma katika taasisi za kiserikali.
"Katika taasisi zenu wananchi wanapokuja kupata huduma huwa kila siku wanaambiwa njoo kesho njoo kesho hiin sasa iondoke,wananchi wapate majibu kutokana na kazi inayofanyika na kwa mambo yenye maslahi ya umma yasicheleweshwe,"alifafanua Rais Dk.Mwinyi.
Katika hatua nyingine Dk. Mwinyi aliwataka wawe wepesi wa kuleta mapendekezo ya sheria pale sheria husika inakuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yapo.
Aidha,Dk. Mwinyi aliendelea kwa kuwataka mawaziri hao wawe wanatoa taarifa zinazofanywa na wizara zao kwa vyombo vya habari ikiwemo mafanikio na changamoto ndani ya wizara hizo.
"Nataka kuwaambia kwamba kuweni marafiki na vyombo vya habari, muwaeleze yale yote mafanikio katika wizara zenu pamoja na changamoto zenu," alisema Dk. Mwinyi.
Aliwasisitiza kusikiliza Malalamiko ya watu huku akiwaambia kwamba kila wizara ihakikishe inaweka utaribu maalumu wa kusikiliza malalamiko ya watu kwa kutumia teknologia zilizopo.
"Jambo la kumi na 13 Usafi, hakikisheni Wizara na taasisi zenu zinakuwa katika hali ya usafi maana baadhi ya ofisi ni chafu zipo kama stoo, hivyo hakikisheni maeneo yenu ya kazi yanakuwa masafi.
Aidha akisisitiza jambo la usafi Dk.Mwinyi alisema kwamba Miji ni michafu haina hadhi hivyo watafute njia mbadala ya kubadilisha hali hiyo ya uchafu na miji kuwa misafi.
Hata hivyo Dk. Mwinyi aliwaambia mawaziri hao kwamba atatembelea kila wizara na kuwapa maelezo ya kina kwa wizara moja moja.
"Nitakuja mwenyewe kwa kila wizara kupata maelezo, matumaini yangu kwamba Ninewateua na nina matumaini nanyi. Nendeni ofisini mkafanye kazi. Yaliyopo nje ya uwezo naa malaka yenu yaleteni kwangu," alieleza Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi.
Dkt Mwinyi. Kwa Uteuzi huu, Ni kielelez
ReplyDeleteo tosha kuwa Umedhamiria na umejipanga
kwa yajayoni Neema na Zanzibar mpya
inakuja.
Hakuna cha Muhali wala Kumuonea mtu haya...katika kutimiza wajibu wake.
Na Kama ni Jipu.!! LITATUMBULIWA
Kila alopewa Dhamana awe NA UBUNIFU.